In Summary

• Ombija alikuwa akifanya mahojiano ya kipekee na Odinga juzi ambapo alitaka kubaini ukweli kwa maneno hayo aliyosema ni ya Ole Kanchory.

Trevor Ombija atakiwa kuomba msamaha chini ya siku 7
Image: Facebook, Instagram

Aliyekuwa ajenti mkuu wa kinara wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga, Saitabao Ole Kanchory amesema kuwa ana nia ya kumpeleka mahakamani mwanahabari wa runinga ya Citizen Trevor Ombija kwa kile alisema ni kumnukuu visivyo.

Juzi Odinga alikuwa na mahojiano ya kipekee na Ombija katika runinga ya Citizen ambapo sehemu kubwa ya gumzo hilo ilihusu jinsi matokeo ya kura za uchaguzi wa Agosti 9 yalivyofanyika hadi mihemko ya mahakamani na sasa uchunguzi unaoendelea dhidi ya baadhi ya makamishna wa tume ya IEBC.

Katika mahojiano hayo, Ombija alimrushia swali Odinga akitaka kubaini kama tetesi za kampeni zake kutokuwa na maandalizi mazuri ni kweli, tetesi ambazo Ombija alisema zilitoka kwa ajenti wa Odinga katika uchaguzi huo, Ole Kanchory.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Ole Kanchory alipakia sehemu ya mahojiano hayo ambapo Ombija anasema maneno hayo yalikuwa yake na kusema kuwa mwanahabari huyo alimharibia sherehe zake za Krismasi katika kile alisema ni kumwekelea maneno ambayo hakuyatamka yeye.

Ole Kanchory alitoa makataa ya siku 7 kwa Ombija kuomba radhi rasmi la sivyo ataelekea mahakamani kumshtaki kwa kumwekea maneno ya uongo mdomoni.

“TANGAZO LA NIA YA KUSHITAKI. Likizo Yangu ya Krismasi imekatizwa vibaya na madai ya uwongo na hasidi kutoka kwa @TrevorOmbija kule @citizentvkenya kwamba nilisema etiKampoeni za @RailaOdinga "hazikuwa na mpangilio na kwamba mawakala hawakulipwa". Isipokuwa nipokee msamaha sawia baada ya siku 7, nitakwenda kushtaki,” Ole Kanchory alitweet.

Aliambatanisha video ya Trevor Ombija akimhoji kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement Raila Odinga ambapo alitaka kuthibitisha kutoka kwa Raila ikiwa madai ya Saitabao kwamba kampeni zake hazikuwa na mpangilio, kituo chake cha kamandi hakikufanya kazi na ikiwa maajenti wake hawakulipwa.

Raila, katika majibu yake, alisema kuwa kampeni ya Azimio zilikuwa mojawapo bora na zilizoandaliwa zaidi nchini; na kwamba walijua ni wapi mambo yalienda vibaya kwao.

 

View Comments