In Summary

• Kujiuzulu kwake kulifuatia joto kali la kisiasa ambalo tume ya IEBC ilijipata ikiogelea ndani mwake.

• Akombe akiwa Marekani alisema hakuwa anajihisi salama kabisa kurejea nyumbani kufuatia vitisho vingi kwa maisha yake.

Roselyn Akombe, aliyekuwa kamishna wa IEBC
Image: Twitter

Aliyekuwa kamishna wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC Dr Roselyn Akombe hatimaye amerejea nchini baada ya kuwa uhamishoni kwa miaka 6 kufuatia joto kali lililohusisha tume hiyo baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.

Akombe alitoroka nchini na kuelekea Marekani siku chache tu baada ya mahakama ya upeo kipindi kile ikiongozwa na aliyekuwa jaji mkuu David Maraga kutupilia mbali ushindi wa rais Kenyatta na kutaka tume hiyo kuandaa uchaguzi wa urais upya ndani ya siku 60.

Akombe baada ya kutoroka nchini kufuatia joto kali la kisiasa lililowekwa na kinara wa NASA kipindi hicho Raila Odinga kupinga baadhi ya makamishna hao kuandaa uchaguzi wa marudio, alitangaza kujiuzulu wadhifa wake akiwa Marekani.

Kutoroka kwake kulifuatia woga uliokuwa umetanda haswa baada ya tume ya IEBC kujipata katikati mwa joto kali la kisiasa, lakini pia kufuatia kifo cha aliyekuwa mkuu wa kitengo cha ICT, Chris Musando kuuawa siku chache kuelekea uchaguzi huo.

Baadae alifanya msururu wa mahojiano ya ufichuzi mkali na vyombo vya habari vya kimataifa ambapo alisema hakuwa anajihisi salama kabisa kurudi nyumbani kufuatia kile alichokiita mikwara mingi kutoka kwa watu ambao hakuwataja kwa majina.

Baada ya kurudi nyumbani, Akombe hakusita kuonesha furaha yake ambapo alipakia picha kwenye ukurasa wake wa Twitter na kusema kuwa hakuna sehemu ya kutia furaha na faraja ya utoshelezi moyoni mwake kama kuwa nyumbani.

“Hakuna sehemu iliyo kama nyumbani Kenya,” Akombe aliandika.

Watu mbalimbali walimkaribisha nchini na kumtaka kujihisi salama kwani nyakati za kupokea vitisho zilishapitwa na wakati.

Ujio wa Akombe unakuja wakati ambapo tume ya IEBC tena imejikuta katika jungu kuu la joto la kisiasa ambapo makamishna 3 kati ya 4 ambao walisimamishwa kazi na rais Ruto ili kutoa nafasi kwa uchunguzi dhidi yao kukamilika, wakiwa wamejiuzulu.

View Comments