In Summary

• Odinga alielekea Nigeria kuhudhuria kongamano la kutoa tuzo kwa uongozi bora barani.

Raila Odinga aondoka kwenda Nigeria
Image: Facebook//Raila Odinga

Kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga ameondoka kwenda ziara ya kikazi nchini Nigeria Afrika Magharibi siku moja baada ya kukiwasha katika uwanja wa Jacaranda jijini Nairobi.

Kinara huyo ambaye amerejelea mikusanyiko yake ya kisiasa kwa wiki moja iliyopita tangu kurejea kutoka ziara nyingine ya kikazi Afrika Kusini alikokwenda kama mjumbe wa muungano wa Afrika kuhusu miundombinu, alidokeza kwenye mitandao yake ya kijamii kwamba ametua Nigeria salama salimini.

Odinga alidokeza kwamba ziara yake katika taifa hilo lenye watu wengi baranai Afrika ni kwa ajili ya kongamano la Tuzo kwa uongozi bora ambalo linafanyika leo hii Jumanne.

“Ninajisikia vizuri kuwa Abuja, Nigeria kwa Kongamano na Tuzo za Uongozi za 2022 kesho! Hebu tujifunze, tuungane, na tusherehekee pamoja,” Odinga alidokeza kwenye picha hiyo akiandamana na viongozi wengine akiwemo aliyekuwa msemaji wa Azimio kipindi cha kampeni, profesa Makau Mutua.

Kuondoka kwake nchini kunakuja siku moja tu baada ya kuwahutubia maelfu ya wafuasi wake katika uwanja mdogo wa Jacaranda Jumapili, akisisitiza msimamo wake kwamba aliibiwa kura katika uchaguzi wa Agosti mwaka jana hivyo hawezi kumtambua Ruto kama kiongozi halali wa taifa.

Kufuatia madai hayo kwamba wana mtoa taarifa wa kuaminika kutoka tume ya IEBC ambaye aliwahakikishia kwa udhibitisho wa hati halali kwamab alishinda uchaguzi huo kwa kura milioni 8 na ushee dhidi ya zile za Ruto ambazo kulingana na mtoa taarifa zilikuwa milioni 6.

Odinga alisema makamishna wa IEBC walibatilisha ushindi wake na kumpa Ruto, na wito wake kwa kiongozi huyo wa taifa ulikuwa kumtaka amuondokee ikulu ili yeye aingie kama rais kwani Wakenya walimchagua yeye lakini IEBC ikawapa kiongozi mwingine.

“Kubali kuwa ulishindwa kwenye uchaguzi, toka Ikulu ili Baba aingie, tunasema ukweli, hatutaki vita, na wala hatutaki vitisho. Tuna haki zetu kama Wakenya, na haiwezi kuporwa na mwewe, Wakenya wanastahili kiongozi waliyemchagua,” alisema.

Odinga aliapa kuendeleza mikutano ya kisiasa kumshinikiza Ruto kumuondokea ikulu, huku safari hii akifutilia mbali uwezekano wa kufanyika kwa maridhiano ya handshake na Ruto kama ilivyofanyika na rais wa awali Uhuru Kenyatta.

 

View Comments