In Summary

• Wakazi walisema makaburi yalikuwa mita chache kutoka kwa makafani ya hospitali ya Mweru ambapo walikuwa wanavuka barabara kuelekea pale.

• Miili hiyo ipatao zaidi ya 140 ilianza kuzikwa alfajiri ya Jumamosi na kukamilika saa mbili asubuhi.

Chumba cha kuhifadhi maiti
Image: BBC

Wakazi wanaoishi karibu na makafani ya hospitali ya rufaa ya Meru walipigwa na butwaa na jinsi wahudumu wa chumba hicho cha kuhifadhi maiti walikuwa wanaendesha shughuli ya kutupa miili ambayo ilikuwa imekaa muda mrefu pasi na kutambuliwa na wenyewe.

Hospitali ya rufaa ya Meru ilitangaza siku chache zilizopita kuhusu mpango wao wa kutupa miili iliyokosa wenyewe, ipatayo 143 katika kaburi la jumla.

Kulingana na taarifa kutoka kwa wakazi walioshuhudia kisa hicho cha ajabu, wahudumu walikuwa wanabeba mwili juu ya machela na kuvuka nayo barabara, mita chache kuelekea kwa makaburi ya jumla ambapo miili hiyo ilikuwa inatupwa.

Miili hiyo ilikuwa inabebwa pasi na kufunikwa huku ikivushwa barabara kwenda kuzikwa.

Zoezi hilo liliripotiwa kuanza mapema alfajiri ya Jumamosi na kukamilika mwendo was aa mbili asubuhi huku baadhi ya walioshuhudia kisa hicho wakipigwa na butwaa ya karne.

Hospitali hiyo katika taarifa yao ya wiki jana ambayo ilipeperushwa kwenye vyombo vya habari, walisema walikuwa na nafasi ya kuhifadhi miili ya watu 60 lakini kufikia kipindi hicho miili Zaidi ya 100 ilikuwa imerundika hapo, na hivyo kutoa makataa ya kutambuliwa la sivyo itupwe kwenye kaburi la jumla kama watu wasiotambulika.

Kaunti ya Nairobi pia siku kadhaa zilizopita walitangaza mpango wa kuzika miili Zaidi ya 290 kwenye kaburi la jumla endapo haingepata utambuzi na wenyewe chini ya siku saba.

Katika kaunti ya Nairobi, makafani ya City yanaongoza kwa miili isiyo na wenyewe, huku uongozi ukisema wengi wa marehemu hao ni wale waliopata ajali barabarani, kuuawa na halaiki ya watu kufuatia visa vya ujambazi na wengine kujitoa uhai.

 

View Comments