In Summary

• Rais alimuagiza Kindiki kuhama ofisi ya Nairobi na kukita kambi bonde la ufa hadi suala la wizi wa mifugo utakapoisha.

Ruto ampa Kindiki mtihani mgumu wa maisha
Image: Facebook

Rais William Ruto amemuamuru waziri wa usalama wa ndani profesa Kithure Kindiki kuhama kutoka kwa ofisi yake jijini Nairobi na kwenda kuishi maeneo ya Bonde la Ufa mpaka pale suala la wizi wa mifugo na ujambazi litakapomalizika.

Katika ibada ya Jumapili iliyoleta pamoja madhehebu mbalimbali kaunti ya Nakuru, Ruto alidhibitisha kutoa agizo hilo ambalo waziri Kindiki anafaa kulitekeleza mara moja bila visingizio.

“Kwa sababu ako pale kwa hiyo sehemu, eo alikwua Baringo, Jana alikuwa Turkana, nimemuambia waziri profesa Kithure Kindiki atoke katika ofisi Nairobi, aende akaishi Bonde la Ufa Kaksazini mpaka pale suala la vifo vya wananchi vitokanavyo na wizi wa mifugo na ujambazi vitakamilika,” rais alifoka.

Alisema kwamba serikali yake imeendelea kuweka mipango kabambe na uwezo mkubwa kuhakikisha kwamba wale wachache wanaojaribu kuonesha kiburi kwa kuendeleza wizi wa mifugo watatokomezwa mara moja.

“Sisi tutapimana na wao na kuhakikisha kwamab hakuna Mkenya atapoteza maisha yake. Wakijaribu kuharibu usalama wa Kenya, tutapambana na wao vilivyo,” rais alisema vikali.

Agizo hili la rais linakuja saa chache baada ya ripoti za ukakasi kutoka Turkana kudai kwamba maafisa wa polisi wa GSU waliokuwa wakipambana wezi wa mifugo eneo hilo walivamiwa na kupoteza maisha yao.

Viongozi kutoka kanda la Bonde la Ufa wamekuwa wakitoa wito kwa rais Ruto kutangaza wazi suala la wizi wa mifugo kuwa ujambazi wa kimabavu ambao adhabu yake inafaa kuwa kali ili kuhakikisha kwamba eneo hilo linapata usalama wa kudumu kwa mifugo.

Suala la wizi wa mifugo katika eneo la bonde la ufa Kaskazini limekuwa sugu kwa miongo kadhaa na sasa viongozi wanataka litangazwe kama janga ambalo linahitaji kukabiliwa kwa nguvu na ustadi vya vikosi vya majeshi ya KDF na si maafisa wa akiba wakisaidiana na wale wa AP na GSU.

Waziri Kindiki amekuwa akifanya ziara na mikutano katika maeneo mbalimbali ya North Rift kutafuta suluhu ya kumalizika kwa wizi wa mifugo lakini magenge hayo wamekuwa wakijibu kwa kutekeleza wizi na mauaji pindi baada ya Kindiki kuondoka.

View Comments