In Summary

• Kufanya taratibu za upandikizaji wa viungo katika taifa hilo pia kutawapunguzia mzigo wa kifedha familia nyingi wakati wa kufanya taratibu hizi nje ya nchi.

Rwanda kuanza kuvuna viungo vya mwili kutoka kwa watu waliokufa.
Image: BBC NEWS

Wizara ya afya nchini Rwanda imesema kwamba sheria mpya ya kuwaruhusu wananchi wa taifa hilo la ukanda wa Afrika Mashariki kutoa viungo vyao muhimu kama msaada baada ya kufa itaanza kufanya kazi mwezi Mei mwaka huu.

Ikiidhinishwa na bunge mapema mwaka huu, 'sheria ya matumizi ya viungo vya binadamu, tishu na seli' inatoa miongozo juu ya mchakato wa uchangiaji viungo vya Wanyarwanda wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, na inaangaliwa kama sheria muhimu itakayosaidia huduma za upasuaji wa upandikizaji na programu za ufundishaji nchini.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliotangulia toleo la tano la Ajenda ya Afya Afrika itakayofanyika kati ya Machi 5 hadi 8 mjini Kigali, Waziri wa Afya wan chi hiyo, Dk. Sabin Nsanzimana, alisema: “Sheria hiyo inatarajiwa kutangazwa kwenye gazeti la serikali katika wiki chache pengine, inategemea. Lakini hatua nyingi zimepitishwa angalau ili tuweze kufanya huduma hizi za upandikizaji bila changamoto zozote za kisheria.”

Alibainisha kuwa baada ya sheria hiyo kuanza kutekelezwa, upandikizaji wa figo unatarajiwa kuanza katika Hospitali ya King Faisal mjini Kigali karibu Mei.

Imefahamika kuwa zoezi la uvunaji wa viungo kutoka kwa wanaotaka kuchangia viungo vyao baada ya kufariki linatarajiwa kuanza hivi karibuni, huku taasisi husika hivi sasa zikifanya maandalizi stahiki kwa taratibu zitakazofanyika kwa mafanikio nchini.

Kufanya taratibu za upandikizaji wa viungo katika taifa hilo pia kutawapunguzia mzigo wa kifedha familia nyingi wakati wa kufanya taratibu hizi nje ya nchi.

View Comments