In Summary

• Kiongozi wa kundi hilo alisema kwamba alikutana na raia wa Kigeni Machakos ambaye alimuahidi kulipa gharama ya hoteli lakini hakuweza kupatikana kwa simu.

• Aliomba mahakama kuwaachia wenzake wawili akisema kuwa hawana hatia bali ndiye mbeba lawama aliyewaalika.

Mahakama
Image: MAHAKAMA

Kisa cha kuchekesha kilijiri katika mahakama ya Eldoret baada ya watu watatu kufikishwa hapo wakishtakiwa kuishi kwenye chumba cha hoteli yenye hadhi ya nyota tatu kwa siku 41 ila kulipa.

Watatu hao, akiwemo mmoja aliyedai kuwa pasta, walisema walipata maono kutoka kwa Mungu akiwaelekeza kwenda Eldoret na kuomba dhidi ya magaidi, na amani, huku nchi ikipitia nyakati ngumu kiuchumi.

Walikuwa wametumia siku 41 kwenye hoteli hiyo ya nyota tatu, wakisali mchana na usiku, hadi wasimamizi wa hoteli hiyo waliposhindwa kuvumilia tena na kuwafanya wakamatwe.

Walikaa katika chumba kimoja chenye vitanda viwili, na kuzungushwa kati ya vyumba mbalimbali.

Bw Alex Muimi Munyoki, 39, Bw Gilbert Muzami Mukisa, 32, na Bi Lilian Namangasa Walukana walishtakiwa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Eldoret Richard Odenyo.

Mahakama ilisikia kwamba mnamo Februari 15, 2023, washtakiwa walidaiwa deni katika Hoteli ya Goshen Inn kwa kupata kiasi cha mkopo cha Sh371,500 kwa kusingizia kuwa mfadhili kutoka Marekani angelipa deni hilo.

Bw Munyoki, kiongozi wa kundi hilo, alisema mfadhili kutoka Marekani aliyetambulika kwa jina la Bw Rooney, ambaye alidai kukutana naye katika mji wa Machakos, aliahidi kulipa bili ya hoteli hiyo, lakini juhudi zake za kufikia mfadhili wake kupitia simu ya rununu ziliambulia patupu.

Bw Munyoki aliambia maafisa wa upelelezi kwamba mnamo Februari 15, Mungu alimwelekeza katika hoteli ya Goshen, ambako alipanga chumba kwa ajili ya kundi hilo kuanza kusali na kufunga kwa ajili ya nchi hadi Machi 28.

Baada ya kukanusha mashtaka, Bw Munyoki aliomba mahakama iwaachilie washirika wake wawili wa maombi akidai alipe gharama hiyo kwa vile aliwaalika wajiunge naye baada ya kukutana nao katika Kituo cha Maombi cha Kaburengu, Kaunti ya Kakamega.

“Naiomba mahakama hii iwaachilie hawa wawili kwa kuwa mimi ndiye mbeba maono. Walikuja tu kuniunga mkono baada ya kuwaalika hotelini,” aliambia mahakama.

View Comments