In Summary

• "Tukalala lakini Kufika usiku mtoto akaanza kuto pofu kwa pua ndio nikaona huyu mtoto bado anahisi vibaya" - Kemunto alisimulia kwa uchungu.

• Jumatatu Kibera ilifurikwa na moshi wa vitoa machozi baada ya polisi kumenyana na vijana wa kutupa mawe wakati Odinga alipeleka maandamano yake mtaani humo.

Image: TWITTER// DCI

Familia moja katika mtaa wa mabanda wa Kibera imetupwa katika kipindi cha maombolezo kufuatia kifo cha mwanao wa miezi minne kutokana na kile walisema ni kuzidiwa na moshi wa vitoa machozi.

Jumatatu wiki hii, maandamano ambayo yameitishwa kote nchini na kinara wa Azimio, Raila Odinga yalianzia mtaa wa Kawangware kabla ya kuelekea Kibera ambapo vijana walimenyana na polisi wa kutuliza ghasia na kupelekea mali ya thamani nyingi kuharibiwa.

Mtaani Kibera ambako kwa muda mrefu kumejulikana kama ngome ya kisiasa ya Odinga kulishuhudiwa machafuko, huku kanisa na msikiti zikitekelezwa na makundi kinzani.

Familia ya Joyce Kemunto ni moja ya wale ambao wanaendelea kuhesabu hasara, si ya mali bali ya maisha kupotea.

Kulingana na Kemunto ambaye aliongea na runinga ya Citizen akiwa na simanzi kuu, yeye hakushiriki maandamano na mwanawe bali ule moshi wa vitoa machozi ulipenyeza hadi kwa nyumba yake, kutokana na kwamba vitoa machozi vilitupwa vingi sana siku hiyo ya maandamano kuwatawanya vijana.

Mtoto wangu ameaga na hakuwa mgonjwa. Na mimi sikuwa maandamano, nilikuwa kwangu kwa nyumba,” Kemunto alisema baina ya kilio.

Mama huyo alisema kwamba moshi ulipenyeza hadi kwa nyumba yake duni na mtoto alianza kukohoa wakadhani ni kikohozi cha kawaida, lakini hali ilikuwa mbaya Zaidi usiku.

“Nilichukua maji nikaweka kwa kitambaa nikaanza kumpangusa uso nikaona mtoto amekuwa sawa. Lakini bado alikuwa analia nikimpangusa uso. Tukalala lakini Kufika usiku mtoto akaanza kuto pofu kwa pua ndio nikaona huyu mtoto bado anahisi vibaya. Sasa ndio nilikuwa nitoke nimpeleke hosipitali akaaga kwa bahati mbaya akafariki,” Kemunto alisimulia.

Licha ya hasara nyingi kushuhudiwa kutokana na maandamano hayo ambayo yamekuwa yakifanyika siku za Jumatatu na Alhamisi, kinara wa ODM Raila Odinga bado ameapa kutolegeza Kamba na Ijumaa akizungumza, alisema kwamba Jumatatu ya wiki kesho ndio kutakuwa na maandamano ya ndovu kumla mwanawe jijini.

Image: TWITTER// DCI
View Comments