Mji wa Eldoret, ambao ni makao makuu ya kaunti ya Uasin Gishu unatarajiwa kupandishwa hadhi kuwa jiji.
Endapo mchakato huu ambao umedokezwa utafaulu kabla ya mwaka huu kuisha, mji wa Eldoret utakuwa jiji la tano la Kenya.
Gavana wa Uasin Gishu Jonathan Bii kupitia ukurasa wake wa Twitter alidokeza kwamba ameteua kamati ya kushughulikia masuala kadhaa ya kutathmini iwapo mji huo umeafikia vigezo vyote vya kupandishwa hadhi kuwa jiji.
“Kuinua Eldoret hadi jiji kutaleta manufaa mengi kwa jumuiya yetu. Itavutia uwekezaji mpya na kuunda nafasi za kazi kwa wakazi wetu, kuboresha miundombinu katika mji wetu, ikiwa ni pamoja na barabara, usafiri na huduma za umma,” gavana Bii alisema.
Gavana Bii alisema tayari mapendekezo ya kamati hayo yamedhihirisha utayarifu wa asilimia 93 wa mji wa Eldoret kupandishwa hadhi.
Bii alithibitisha kuwa wanawake, vijana, Watu Wenye Ulemavu (Walemavu), vyama jirani vya wakazi, Wabunge wa Bunge la Kaunti na wenzao wa Bunge la Kitaifa wote walipewa fursa ya kutoa maoni yao.
“Kamati iliyopewa jukumu la kutafuta maoni kuhusu iwapo Manispaa ya Eldoret inapaswa kuinuliwa hadi hadhi ya jiji leo imetoa uamuzi, "NDIYO" kali kwa "Jiji Jipya la Mabingwa" kwa kiwango cha kuidhinishwa kwa asilimia 93,” gavana Bii alisema.
Lakini je, unafahamu baadhi ya vigezo vinavyohitajika ili mji kupewa hadhi ya jiji?
Kwa mji kupewa hadhi kuwa jiji, ni sharti idadi ya watu iwe angalau laki mbili na nusu, vyuo vya masomo, uwepo wa viwanja vya ndege, masoko ya kisasa, barabara pana zilizoboreshwa na taa miongoni mwa vigezo vingine.
Eldoret utakuwa mjiwa tano kupandishwa hadhi baada ya Nakuru kupewa hadhi hiyo mwaka 2021.
Nairobi, mji mkuu wa Kenya ulikuwa wa kwanza kupewa hadhi ya kuwa jiji mwaka 1950 na kufuatiwa na Mombasa na Kisumu baadae.