Uongozi wa kaunti ya Nairobi umeanzisha mchakato wa kubadilisha magari makuukuu ya askari wa kaunti almaarufu kanju na magari mapya.
Kwa muda mrefu, Kanju wamekuwa wakijulikana kupiga misele katika mitaa mbalimbali ya jiji la Nairobi kwa kutumia magari hayo ya kitambo ambayo yamefunikwa lakini sasa magari hayo yameanza kubadilishwa na mapya ambayo ni aina ya pick-up.
Kupitia ukurasa wa Twitter, uongozi wa kaunti ya Nairobi walisema kwamba mchakato huo umeanzishwa ili kuipa idara ya kanju sura mpya.
“Tunaondoa polepole magari ya zamani na kuchukua nafasi ya magari mapya. Lazima iWork,” uongozi wa kaunti ulidokeza, ukipakia picha za muonekano wa magari hayo mapya.
Kando na kubadilisha magari hayo ya Kanju, serikali ya kaunti hiyo pia ilitangaza kununua magari matatu yenye uwezo wa kufagia barabara za jiji pamoja pia na kuwa na mfumo wenye uwezo wa kuzoa taka.
“Lori la kufagia barabarani lina vifaa kamili vya taka, pipa la kukusanya vumbi, na mfumo wa kusafisha. Ni moja ya malori matatu (3) ya ubora wa juu ya kufagia barabara ambayo Gavana @SakajaJohnson amewekeza, ili kuleta utulivu na heshima katika jiji. Lori hili linatumika sana katika kusafisha na kusugua usiku na jioni. Linatumia mchanganyiko wa kusugua na kusafisha kwa shinikizo la juu. Barabara zinazosafishwa kwa sasa na mfagiaji barabara usiku huu ni pamoja na Moi Avenue; Tom mboya Street, na Haileselasie Avenue,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma huku lori hilo likionekana kazini usiku wa Jumanne.