In Summary

• Kulingana na DCI, asubuhi hiyo ya tukio, mshukiwa alitoka nyumbani na kwenda kazini kama kawaida.

• Aliwafahamisha wenzake kwamba marehemu alikuwa ameacha kazi yake na wangehama nyumba yao na kwenda kusikojulikana.

Morris Njuguna amefichua sababu ya kumuua mpenzi wake, kuweka mwili kwa gunia.
Image: Facebook//DCI

Wiki moja baada ya mwanamume mmoja Morris Njuguna mwenye umri wa miaka 28 kutoka Ruiru kukiri kwamba ndiye alihusika katika mauaji ya mkewe Risper Ndunge na kuupakia mwili wake ndani ya gunia, DCI wamebaini sababu ya Njuguna kutekeleza unyama huo.

Katika sasisho la kina ambalo Idara ya DCI ilichapisho kwenye ukurasa wao wa Facebook, walisema kuwa baada ya kumhoji kwa muda Njuguna, aliwaambia kuwa mkewe alifika nyumbani saa tisa alfajiri, jambo lililogeuka kuwa sababu ya ugomvi wao.

“Hata hivyo, kutokana na aina ya majukumu yao, mwanamume huyo ndiye angekuwa wa kwanza kufika nyumbani kabla ya saa nne usiku, wakati marehemu angefikishwa nyumbani baadaye saa za usiku mkuu, saa tisa asubuhi. Hili halikuwa sawa kwa Morris ambaye alishuku kuwa wakati huo wote haukutumika kusawazisha mauzo ya siku kama inavyodaiwa, lakini kwa shughuli zingine za kutiliwa shaka,” sehemu ya sasisho la DCI ilisoma.

Mwili wa Ndunge uligunduliwa kwenye lango la jengo la kukodisha na wapangaji wa Mitikenda eneo la Gatongora huko Ruiru, na kusababisha wapelelezi kuanzisha uchunguzi mara moja kuhusu tukio hilo la kushangaza.

Marehemu ambaye alifanya kazi kama keshia katika mkahawa wenye shughuli nyingi wa nyama choma ulioko Kamakis kando ya njia ya Mashariki, alikuwa amehamia kwa mchumba wake Morris Njuguna, 28, ambaye ni mpishi katika kituo hicho miezi michache iliyopita.

Tayari wapelelezi wamedhibitisha kwamba wamepata haki ya kutumia ushahidi wa mkanda wa CCTV katika uchunguzi wao ili kufichua ukweli wote na kupata ushahidi tosha kabla ya Njuguna kufunguliwa mashtaka.

Kulingana na DCI, asubuhi hiyo ya tukio, mshukiwa alitoka nyumbani na kwenda kazini kama kawaida. Aliwafahamisha wenzake kwamba marehemu alikuwa ameacha kazi yake na wangehama nyumba yao na kwenda kusikojulikana.

Jioni hiyo, mshukiwa alirudi nyumbani akiwa amebeba gunia ambalo alikuwa amenunua mapema mchana. Aliuweka mwili wa marehemu kwenye sanduku la kusafiria kabla ya kuufunika kwa gunia.

Kisha mshukiwa alibeba mwili wa marehemu ukiwa umejificha kama mzigo, na baada ya kilomita moja, akautupa nje ya lango, kabla ya kuondoka.

Picha za CCTV zilizopatikana na maafisa wa upelelezi zilionyesha mshukiwa akiwa amebeba gunia hilo mwendo wa saa tatu na nusu usiku kabla ya kulitupa.

Ugunduzi wa kushangaza wa mwili wa marehemu uliripotiwa katika kituo cha polisi cha Gatongora na mwenye nyumba wa jengo lililo karibu na mahali ambapo mabaki ya Ndunge yalitupwa.

View Comments