In Summary

• Wazee hao walisema wametoa maonyo kadhaa kwa vijana katika jamii kutoandamana lakini maombi yao hayajatekelezwa.

KINARA WA AZIMIO RAILA ODINGA
Image: ANDREW KASUKU

Huku kiongozi wa mrengo wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya ukijiandaa kujitosa barabarani kwa mkumbo wa pili wa maandamano baada ya kusitishwa kwa takribani mwezi mmoja, wazee kutoka jamii ya Luo wameapa kutamka laana kali kwa yeyote atakayeitikia wito wa kuandamana.

Wazee hao walisema wametoa maonyo kadhaa kwa vijana katika jamii kutoandamana lakini maombi yao hayajatekelezwa.

Katika taarifa iliyopeperushwa na runinga ya NTV, wazee hao walisema kuwa yeyote atakayeitikia wito wa Odinga kujitosa kwenye maandamano dhidi ya serikali ataandamwa na laana hiyo kali.

“Wazee wanajulikana kuwa watu wanaotetea amani. Tayari tumehisi hatari na kuwataka vijana wasiandamane,” mzee Nyandiko Ongadi ambaye ni mwenyekiti wa baraza la wazee wa Kijaluo alisema.

Mzee huyo aliwataka wanajamii wa Luo kuwakanya watoto wao kutojihusisha na maandamano hayo huku pia akiutetea uongozi wa rais Ruto.

"Kenya inaweza kutumbukia katika machafuko ikiwa upinzani utaendelea na mipango yake ya maandamano," Bw Ongadi alisema.

Naibu wake Thomas Achando alitoa wito kwa wanajamii wake kufanya kazi na serikali ikiwa wanataka masuala yanayowahusu kutatuliwa.

"Tutumie fursa ya mvua kuwa na tija na usalama wa chakula badala ya kwenda mitaani," alisema.

Walipendekeza Bw Odinga airuhusu timu iliyopewa jukumu la kuongoza mazungumzo ya pande mbili kukamilisha kazi yake kabla ya kuipa nchi matokeo yao.

Wenzao kutoka jamii ya Suba walisema watatumia njia tofauti kutafuta usaidizi kutoka kwa serikali.

Pia wamelaani vitendo vyovyote vya unyanyasaji dhidi ya serikali wakisema havitawaongezea thamani ya kiuchumi, badala yake vinawafanya kuwa maskini zaidi. Wazee hao walizungumza wakati wa mkutano katika ofisi ya baraza hilo iliyopo Sindo Mjini.

View Comments