In Summary

• Mfanyibiashara huyo alisema aliitwa na DCI ambao walimuitisha logbook ya gari hilo na kumwambia watampigia simu baada ya uchunguzi.

• Gari hilo la kubeba abiria 33 liliteketezwa Ngong Road wakati wa maandamano Jumanne.

Basi la abiria lililochomwa Ngong Road wakati wa maandamano.
Image: Maktaba

Jumanne Mei 2, mrengo wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya ulirejelea duru ya pili ya maandamano baada ya kusitishwa takribani mwezi mmoja uliopita.

Katika maandamano hayo ambayo hata hivyo vinara wakuu hawakushiriki, visa mbalimbali vya uhalibifu wa mali ya watu viliripotiwa katika maeneo mengi nchini ambayo Odinga anajivunia kuwa na ufuasi mkubwa.

Jijini Nairobi, magari mawili yaliripotiwa kuchomwa moto na kundi la vijana ambao wanakisiwa kutumia fursa ya maandamano ya Azimio kutekeleza maovu yao.

Katika barabara ya Ngong, basi la lililokuwa likisafirisha watu kuingia jijini lilitiwa moto na kundi la vijana wahalifu ambao kabla ya kulitia moto waliwaibia abiria na kuwajeruhi baadhi yao kwa silaha kali.

Mmiliki wa gari hilo amevunja kimya chake na kusema kwamba dereva alimpigia simu akilia na yeye alikuwa katika hafla ya mazishi.

Jamaa huyo mwenye umri wa makamo alizungumza kwa uchungu akisema kwamba gari hilo lilikuwa ndio tegemo kubwa kwa familia yake na pia alikuwa bado anaendelea kulipia riba ya mkopo.

“Nilikuwa mazishi mahali, nikapigiwa simu na dereva na akaniambia kuwa amepatana na wahalifu huko Posta Ngong Road na akatolewa kwa gari akapigwa. Alikuwa Analia mimi nikamwambia wewe usijali,” mwanamume huyo alisema.

Alisema kuwa baadae aliitwa na makachero wa idara ya DCI ambao baada ya usaili wa muda walitaka kubaini umiliki wa gari hilo ambapo walimuomba hati na kumpa matumaini kuwa wataendelea na uchunguzi.

“Niliitwa na DCI waliniitisha logbook na wakasema watanipigia. Sasa mimi hilo gari ndilo lilikuwa linalea familia na sasa sijui vile nitafanya na hilo gari lilikuwa la mkopo,” mjasiriamali huyo mwenye uchungu alisema.

Alitoa wito kwa mtu yeyote au serikali kumpa msaada kwa sababu kuchomwa kwa gari hilo kulimsukuma katika sehemu ngumu kimaisha ambapo hawezi jinasua.

“Naomba tu serikali au mtu yeyote atakayejitokeza, tafadhali nimeomba tu usaidizi kwa sababu familia yangu sijui sasa tutafanyaje,” alisema kwa majonzi.

View Comments