In Summary

• "Sasa wameparamia kuripoti tukio moja tu la kufokewa na watu watatu!” Miguna alisema.

Miguna Miguna afunguka kilichosababisha kufurushwa nchini 2018
Image: Facebook

Siku mbizi zilizopita, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii iliripoti kwamba wakili mwenye utata Miguna Miguna alifokewa vibaya na sehemu ya waombolezaji baada ya kujaribu kumzungumzia Raila Odinga kwa njia hasi katika hafla ya mazishi kaunti ya Homa Bay.

Kulingana na taarifa za awali, Miguna alikuwa akiendeleza juhudi zake za kujaribu kumng’atua Odinga kama msemaji wa eneo pana la Nyanza ambayo kwa muda mrefu imekuwa ngome yake ya kisiasa.

Lakini safari hii, wakili huyo aliyerejea nchini kutoka Kanada baada ya kuwa uhamishoni kwa Zaidi ya miaka minne alikiona cha mtema kuni waombolezaji walipokaidia kununua ngonjera zake kuhusu ‘ubaya’ wa Odinga.

Lakini Miguna Miguna maadamu ana mdomo basi kila mmoja alitarajia kwa namna yoyote tu lazima angezungumzia tukio hilo na kujiweka katika upande chanya wa kilichotokea.

Ni kweli. Miguna kupitia Twitter yake juzi amezungumza na kwa kujitetea, amevitupa vyombo vya habari kwenye reli ya treni akisema kuwa ndio waliripoti kwa njia ya uchochezi.

Kwa mujibu wa wakili huyo, katika harakati zake dhidi ya Odinga kwenye eneo la Nyanza, alishangiliwa kwa mbwembwe tele katika maeneo 3 ambayo ni ngome ya Odinga lakini wanahabari hawakuripoti, ila lilipotokea lile la kufokewa na umati wa watu aliowataja kuwa watatu, kila chombo cha habari kiliparamia kuripoti.

“Githeri Media inatabirika sana. Nilishangiliwa sana katika hafla 3 huko Nyando, Nyakach na Muhoroni wiki iliyopita baada ya kupiga kelele hadharani dhidi ya @RailaOdinga lakini Githeri Media haikuripoti hayo hata kwa sentensi moja. Sasa wameparamia kuripoti tukio moja tu la kufokewa na watu watatu!” Miguna alisema.

View Comments