Naibu Rais Rigathi Gachagua Jumatano katika hafla ya maombi ya kitaifa alifahamisha umma kuwa jina lake la ubatizo ni Geoffrey lakini aliacha kulitumia miaka mingi iliyopita.
Naibu huyo wa rais mwenye kusema sana kwa mara ya kwanza alifunguka sababu za kuacha kutumia jina hilo licha ya kwamba ndilo jina la Ubatizo wake.
Gachagua alisema kuwa mara nyingi alikuwa akilitumia jina hilo wakati anahudumu kwenye utumishi wa umma kama DO lakini baada ya kubadilisha kazi, alilazimika pia kuliasi jina hilo.
Gachagua alikuwa anajaribu kufafanua na kunyoosha maelezo kuhusu ukaribu wake na dini na kuwatoa wasiwasi kuwa yeye ni Mkristo aliyebatizwa.
“Kwa wale ambao pengine wanatilia shaka imani yangu, kwa sababu sina jina la ubatizo, kwa hakika nilibatizwa na jina langu ni Geoffrey.”
“Nilipokuwa naitwa Geoffrey nilikuwa msimamizi wa kutawala watu. Nilipobadilisha maelezo yangu ya kazi ili kuwatumikia wananchi, nilihitaji kubadili jina langu ili nibadilishe utambulisho wangu katika maelezo yangu mapya ya kazi,” alisema.
Akiongeza: “Ili ujue kwamba mimi ni Mkristo kikweli, una uthibitisho kwamba nimemuoa mchungaji.”
Mnamo mwaka 2022 baada ya uchaguzi mkuu, Gachagua alifurahia baada ya kuitwa kwa jina la majazi Riggy G ambalo lilibuniwa na mrembo Ivy Chelimo.
Naibu wa rais aliwashangaza wengi alipotaka kukutana na mrembo huyo na baadae akampa kazi katika ofisi ya naibu wa rais.
Taasisi ya Kenya Industrial Property (KIPI) ilithibitisha kwamba Gachagua alituma maombi ya kupata hatimiliki ya jina hilo mnamo Novemba 10, 2022, na kuwazuia watu wengine kutumia jina hilo bila idhini yake.