In Summary

• Ikumbukwe Kuria wiki mbili zilizopita alikuwa amekunjiana mashati na kampuni ya vyombo vya habari ya Nation.

Image: Instagram, Facebook

Waziri wa viwanda na biashara Moses Kuria ametoa malalamiko yake kwa vyombo vya habari kwa kutoangazia habari za kurauka kwake alfajiri na mapema kila siku.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Kuria alilalamika kwamba licha ya kurauka kila siku alfajiri ya saa tisa ili kujitahidi kufanya mambo makubwa ya kuboresha uchumi, hakuna media inaripoti kuhusu hilo.

“Kila siku huwa narauka mapema sana ya saa tisa asubuhi kufanya mambo ya ajabu ili kuboresha uchumi. Vyombo vya habari haviwezi kuripoti kuhusu hilo. Kwa hiyo nimeamua kufanya tu,” Kuria aliandika.

Waziri huyo mbatukaji aliendelea kusema kuwa ameamua naye kufanya kazi yake huku akifumba jicho kwamba haoni kama kuna mtu anayemuona na pengine kutambua jitihada zake katika kuboresha uchumi wa Kenya ambao umekuwa katika hali ya utelezi katika siku za hivi karibuni kutokana na mfumko mkubwa.

“Moja, nitaendelea kufanya kazi yake kuboresha uchumi iwe media wanaripoti au la,” Kuria alisema.

Wengi walihisi ni kama kinaya kwa waziri huyo kutaka media iripoti mambo yake ilhali media hiyo hiyo ndio amekuwa akitupia maneno ya nguoni na kashfa katika wiki mbili zilizopita.

Ikumbukwe Kuria wiki mbili zilizopita alikuwa amekunjiana mashati na kampuni ya vyombo vya habari ya Nation kwa kusema kuwa walikuwa wanalenga kuipaka tope serikali, madai ambayo yalipingwa vikali na baraza la vyombo vya habari MCK lakini pia muungano wa wahariri nchini KUJ.

Hata hivyo, serikali ikiongozwa na naibu rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa wengi katika bunge Kimani Ichung’wah wamekuwa mstari wa mbele kutetea madai ya Kuria wakisema kuwa licha ya kuwepo kwa uhuru wa vyombo vya habari, kuna baadhi ya vyombo hivyo ambavyo vinatumia uhuru huo vibaya, huku wakiitisha uwajibikaji kutoka kwa wanahabari.

View Comments