In Summary

•Raila amefanikiwa kufanya mkutano wa ghafla na kuhutubia wananchi wengi waliojitokeza katikati mwa jiji la Nairobi mapema leo.

•Ijumaa ya wiki jana, gari la Raila Odinga lilidaiwa kupasuliwa kioo cha nyuma, katika kile ambacho alitaja kuwa ilikuwa njama ya kumwuua.

Kinara wa upinzani akiandamana na raia katikakati mwa jiji la Nairobi, Julai 10
Image: Raila Odinga// TWITTER

Kinara wa muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga maarufu Baba amefanikiwa kufanya mkutano wa ghafla na kuhutubia wananchi wengi waliojitokeza katikati mwa jiji la Nairobi mapema leo.

Kiongozi huyo wa upinzani alidai kwamba aliamua kuliacha gari lake katika eneo la Rongai, na badala yake kutumia matatu iliyompeleka hadi katika mwa jiji (CBD) alipokutana na halaiki kubwa ya raia waliokuwa wamemsubiria.

Odinga aliamua kutumia matatu, kama kielelezo kwa wafuasi wake, ambao aliwashauri mapema mwezi huu kwamba watumie matatu au kutembea wanapoelekea kazini ili kuinyima serikali tawala ushuru unaokatwa kwa mafuta ya magari.

Mkuu huyo wa Azimio alionekana akitembea huku akiwa amewekewa ulinzi mkali na maafisa wenye ujuzi mkubwa hadi alipoingia kwenye gari lake la kibinafsi ambapo alianza kuwahutubia raia waliojitokeza.

Katika hotuba yake, Odinga alizungumzia saini milioni 15 ambao muungano huo unadhamiria kuzikusanya kutoka kwa Wakenya ili kuweza kuibandua serikali ya Rais William Ruto mamlakani.

Kwanza nawashukuru sana kwa kujitokeza kwenu siku ya Saba Saba, mlionesha kuwa mna uwezo wa kuweza kujitawala wenyewe. Ningependa tukusanye saini milioni 15 kama dhibitisho tosha kuwa Wakenya wamechoshwa na utawala wa William Ruto na Gachagua,” alieleza Odinga.

Aliendelea kumshutumu Rais Ruto kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili Wakenya kutokana na bei ghali ya bidhaa za matumizi, ambapo aliwaambia raia kuwa wawe tayari siku ya Jumatano wiki hii kwa maandamano ya kuupinga uongozi wa serikali.

Bei ya unga iko juu, bei ya mafuta iko juu, bei ya sukari bila kuisahau. Nilimwambia punda amechoka asiongeze mzigo akataa kusikia. Jumatano mjitokeze kwa wingi, ili tuweze kufanya maandamano ya amani, tutaishinda serikali maana uongozi upo miongoni mwa Wakenya,” Aliendeleza.

Ijumaa ya wiki jana, gari la Raila Odinga lilidaiwa kupasuliwa kioo cha nyuma, kile ambacho alitaja kuwa ilikuwa njama ya kumuua.

Watu wanne kufikia sasa wameripotiwa kufariki dunia na wengine kuendelea kuuguza majeraha baada makabiliano kati ya raia na maafisa wa usalama wakati wa maandamano ya Sabasaba.

View Comments