In Summary

• Seneta huyo alisema kuwa hakutakuwa na vurugu za aina yoyote na kuwataka watu kuendelea na shughuli zao za kila siku.

• Azimio wametangaza maandamano yao ya siku tatu kuanzia asubuhi Jumatano hadi Ijumaa.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei.
Image: STAR

Seneta wa Nandi ambaye ni mtetezi mkali wa sera za rais William Ruto, Samson Cherargei na uongozi wake amesisitiza lengo lao la awali kwamba wakati maandamano ya upinzani yatakuwa yanaendelea kote nchini, naye atawaongoza wenzake kufanya vikao vya Amani katika maboma ya viongozi wakuu wa upinzani, Uhuru Kenyatta na Raila Odinga kote nchini.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Cherargei aliapa kwamba watazuru maboma ya viongozi hao kufanya kile alichokitaja kuwa ni vikao vya Amani kujadili kuhusu mustakabali na mwafaka wa biashara ambazo huenda zitalemazwa wakati wa maandamano hayo ya siku tatu.

“Kama tulivyoahidi kesho tutakuwa na kikao cha Amani katika makazi/nyumba za Tinga/Uhuru kote nchini kuelezea usumbufu wa biashara zetu,” Cherargei alisema.

Seneta huyo mbwatukaji alisema kuwa Jumatano itakuwa siku ya kawaida kote nchini na kuwataka watu woote kutohofu kuhusu biashara au shughuli zao za kila siku kulemazwa na maandamano.

“Kesho ni siku ya KAWAIDA ya kazi kwa Wakenya wote. Tunawahimiza Wakenya kuripoti katika majukumu yao ya kawaida huku tukimaliza mashambulizi ya ndani ya Tinga/Uhuru kesho,” alisema.

Seneta huyo alionekana kuradidi maneno ya bosi wake Ruto kwamba Uhuru Kenyatta ana mkono katika maandamano ambayo yanaendelea kote nchini yanayoongozwa na kinara wa Azimio, Raila Odinga.

Awali, mwanablogu wa serikali Dennis Itumbi alikuwa ameandika ujumbe sawia na huo akilenga kusema kwamba alikuwa anatumai kukutana na yule aliyemtaja kuwa ni mfadhili wa maandamano.

Itumbi alikuwa amesema kwamba Jumatano asubuhi, angependa kuandamana na watu Zaidi ya elfu mbili ili kumfuata mfadhili huyo wa maandamano katika maboma yake nchini ili kuwasilisha ujumbe wao.

“Mpendwa mfadhili mkuu wa Maandamano, ninakuandikia kuweka miadi nyumbani kwako siku ya Jumatano....Nitasindikizwa na watu 2,848 pekee katika kila sehemu unayoweza kuwa. Nairobi. Kiambu. Nakuru. Mombasa. Muthaiga. Trans-Mara. Ajenda ni kujadili jinsi ya kufanya Maandamano kuwa ya ufanisi zaidi. Nina hakika hiyo iko karibu na moyo wako,” sehemu ya ujumbe wa Iutmbi ulisoma.

View Comments