In Summary
  • Akizungumza na vyombo vya habari mnamo Jumanne, Julai 25, alidai kuwa Ruto alimwalika Suluhu nchini Kenya ili kusaidia pande zinazozozana kukubaliana na mapatano.
Kiongozi wa ODM Raila Odinga
Image: TWITTER

Raila Odinga amedai kuwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu alikatishwa tamaa katika juhudi zake za kupatanisha yeye na mkuu wa nchi ya Kenya, William Ruto.

Akizungumza na vyombo vya habari mnamo Jumanne, Julai 25, alidai kuwa Ruto alimwalika Suluhu nchini Kenya ili kusaidia pande zinazozozana kukubaliana na mapatano.

Hata hivyo, alizuiliwa kwa siku chache na utawala wa sasa, hivyo kumlazimu kurejea Tanzania.

"Alijaribu kupatanisha lakini alisubiriwa kwa siku kadhaa na upande mwingine. Upande wetu ulikuwa tayari na unapatikana kwa mazungumzo lakini Serikali ilikataa kujibu," Raila aliambia wanahabari.

Raila alidai, upinzani ulikuwa tayari kukutana na Suluhu na wajumbe wengine wa amani.

Wiki iliyopita, Suluhu alionekana katika Hifadhi ya Taifa ya Maasai Mara, ambako inadaiwa alikutana na wanasiasa kadhaa wa ngazi za juu kutoka muungano wa Azimio la Umoja.

Kiongozi wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) alidai kuwa Ruto alimtendea mwenzake wa Tanzania dharau, jambo ambalo huenda likaathiri pakubwa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili.

“Ni Kenya Kwanza ambayo inakatisha tamaa juhudi zozote za kuleta hali ya akili timamu nchini. Hatupendi kuwa sehemu ya matatizo serikalini, hatutaki kula mkate wao, tunachotaka ni Wakenya tu kuweka chakula mezani," Raila alisema.

 

 

 

 

 

View Comments