In Summary

• Osoro katika hotuba yake alitumia mfano wa bei ya mbolea, bei ya mahindi na bei ya maharagwe ambayo alisisitiza kwa kutumia jina la aina moja ya maharagwe – Rosecoco.

• Rosecoco imekuwa ikitumiwa na vijana humu nchini kama tasfida ya uke.

Osoro amtaka Odinga kutomhusisha rais Suluhu katika masiala ya humu nchini.
Image: Facebook

Mbunge wa Mugirango wa Kusini ambaye pia ndiye kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa Silvanus Osoro kwa mara nyingine yuko kwenye vichwa vya habari mitandaoni kuhusu matamshi yake ya utani na kuchekesha kuhusu madai ya kiongozi wa mrengo wa upinzani Raila Odinga kutaka rais wa nchi jirani kuleta upatanishi nchini.

Osoro akizungumza katika hafla moja alimwambia Odinga kwamba haiwezekani yeye atake kiongozi wa Tanzania rais Samia Suluhu Hassan kuacha kazi ya kuwahudumia Watanzania waliomchagua ili kuja humu nchini kutatua mzozo wa gharama ya juu ya maisha – kwani hilo ni jambo ambalo viongozi wa Kenya wanaweza kufanya bila kusaidiwa.

Osoro katika hotuba yake alitumia mfano wa bei ya mbolea, bei ya mahindi na bei ya maharagwe ambayo alisisitiza kwa kutumia jina la aina moja ya maharagwe – Rosecoco – ambayo humu nchini imekuwa ikitumiwa kama tasfida kuashiria sehemu za siri za wanawake.

“Safari hii tunamwambia mheshimiwa Raila Odinga, kama tunataka kuzungumza juu ya maneno ya gharama ya maisha, hatuhitaji rais Samia Hassan akuje kuongea juu ya bei ya mbolea, au mahindi. Samia Suluhu ako na nchi yake kule Tanzania, wewe ongelelea yako hapa,” Osoro alimwambia Odinga.

“Sasa unataka Samia Suluhu akuje hapa Kenya aketi na mheshimiwa rais Ruto waongee juu ya bei ya maharagwe, siku hizi nasikia maharagwe yanaitwa sijui Rosecoco. Sasa Samia Suluhu akuje kuongelea juu ya bei ya Rosecoco hapa, si ako na Rosecoco yake kule Tanzania, si wacha sisi tuzungumzie juu ya bei ya Rosecoco yetu hapa Kenya, ama namna gani? Si namna hiyo?” Osoro aliongeza huku umati ukimshabikia.

Osoro alikuwa anamjibu Odinga baada ya kudai kwamba wiki mbili zilizopita rais Ruto alimpa rais Suuhu wa kuja nchini ili kuwapatanisha na yeye lakini upatanishi huo haukufanikiwa kwani Suluhu aliachwa kwenye mataa katika hoteli moja kwa siku mbili kabla ya kuamua kurudi nchini mwake.

Odinga alisema haya mapema wiki hii alipokuwa na mkutano na vyombo vya habari vya kimataifa.

Akijibu madai yake, Rais Ruto kupitia Twitter alimwambia Odinga kwamba ndio alikuwa njiani kwenda Tanzania katika shughuli za kiserikali lakini akamhakikishia kwamba atakaporudi nchini, ako tayari kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na yeye, akisema kwamba hata Odinga mwenyewe anajua kuwa yuko tayari muda wowote kufanya mazungumzo naye.

 

View Comments