In Summary

• Mkereketwa huyo wa sera za serikali ya Kenya Kwanza alisema kwamba hatua hiyo itafanya kila Mkenya kujua ni nini viongozi hao watajadili.

Kimani Ichung'wah.
Image: Facebook

Mbunge wa Kikuyu ambaye pia ndiye kiongozi wa walio wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichung’wah ametoa sharti moja kwa rais Ruto pindi watakapokutana na kinara wa upinzani Raila Odinga ili kutafuta mwafaka wa taifa kutokana na maandamano.

Ichung’wah ambaye aliandamana na rais Ruto kule Kilifi katika ziara yake ya wiki moja kwenye mwambao wa Pwani alisema kwamba iwapo wawili hao watakutana, basi isiwe ni mkutano wa faragha bali uwe ni mkutano wa hadharani utakaofuatiliwa moja kwa moja na kila mtu.

Mkereketwa huyo wa sera za serikali ya Kenya Kwanza alisema kwamba hatua hiyo itafanya kila Mkenya kujua ni nini viongozi hao watajadili ili kupata hatima ya kuondoa taifa katika wimbi siasa za maandamano na kutoa nafasi ya uchumi kukua katika mazingira ya Amani.

Ichung’wah pia alisema kuwa hatua hiyo itahakikisha hakutakuwa na mazungumzo ya masuala ya kibinafsi bali ya kumjali kila Mkenya ambaye anaathirika kutokana na mwendelezo wa maandamano ambayo yamekuwa yakiitishwa na Azimio tangu mwezi Machi mwaka huu.

“Wananchi wa Magarini na Kenya mzima wamesema wanataka kuwa mashahidi wa yale mazungumzo ambayo mtakuwa nayo ili pasiwe na mambo ya kibinafsi. Yawe ni mazungumzo ya kufufua uchumi, mamabo yanayohusu wananchi wa kawaida wa Kenya,” alisema Ichung’wah.

Katika mkutano huo, Ruto aliwasuta vikali viongozi wa upinzani ambao walishiriki katika ibada ya kuwakumbuka waandamanaji waliofariki kutokana na maandamano hayo.

Ruto alisema kwamba viongozi wa upinzani wanastahili kuomba Kenya msamaha kwa kuandaa maandamano ambayo yalisababisha maafa, uharibifu wa mali ya umma na biashara za watu

Kiongozi wa taifa alisema kwamba machozi yao si ya kweli kwani kama si wao walioandaa na kufadhili maandamano hayo, basi mali na maisha ya watu hayangepotea.

View Comments