In Summary

• Hata baada ya kufika katika afisi za KUCCPS jijini Nairobi, mwanafunzi huyo hakupata usaidizi akiambiwa arudi wiki kesho.

• Wasiwasi wake sasa ni kwamba wiki kesho atapata kozi zote nzuri zimechukuliwa.

Ezekiel Machogu, waziri wa Elimu.
Image: Twitter//Wizara ya Elimu

Ikiwa ni siku moja tu baada ya wizara ya elimu kutangaza kuachiliwa kwa matokeo ya wahitimu wa mitihani ya KCSE mwaka 2022 kujiunga taasisi za masomo ya juu, tayari wengi wa wanafuzni hao wamejitokeza kwa malalamishi kuhusu uteuzi huo.

Mwanafunzi mmoja binti aliyefuzu kwa alama ya A chanya (-) kutoka shule ya kitaifa ya wasichana ya Pangani ni mmoja wa wale ambao habari zake zimeangaziwa baada ya kuteuliwa kufanya kozi ya astashahada kwenye chuo anuwai, TVET.

Kulingana na ripoti ya runinga ya Citizen, mwanafunzi huyo alikuwa na matumaini makubwa ya kuteuliwa kujiunga na moja ya vyuo vikuu nchini kuendeleza masomo yake ya shahada ya kwanza.

Pindi alipotuma nambari yake ya usajili wa mitihani ya KCSE mwaka jana kwenda kwa kodi iliyotolewa na KUCCPS – taasisi inayotoa uteuzi kwa wanafunzi wa kujiunga na taasisi za masomo ya juu, alipigwa na butwaa kupata kwamba aliteuliwa kusomea kozi ya chuo anuwai TVET badala ya chuo kikuu.

Mwanafunzi huyo mapema Jumanne alielekea katika afisi za KUCCPS kutoa malalamishi yake dhidi ya uteuzi huo ambao alidai si wa haki kwa upande wake kwani alijisatiti masomoni na kupata alama ya A-.

“Waakti ujumbe ulikuja, nilipata kwamba nimeitwa katika shule ya Kiambu Institute kufanya kozi ya lishe bora. Na mimi nikiwa shule ya upili nilipata alama ya A- na nilitarajia kupata kozi ambayo niliichagua,” alisema.

Mwanafunzi huyo hata hivyo hakupata usaidizi aliokuwa akihitaji akiambiwa kwamba nafasi za kupeleka maombi ya kubadilisha kozi zitaanza kufunguliwa wiki kesho.

Wasiwasi wake ni kwamba wiki kesho huenda akapata kozi zote nzuri katika vyuo vikuu zimejaa na hakutakuwa na nafasi ya kupokea wanafunzi wapya.

“Tatizo ni kwamba kozi zote nzuri wiki kesho zitakuwa zimechukuliwa na sasa sijui nitatuma ombi kwa kozi gani au chuo kipi. Kufanya pia kozi ya kujisimamia kwa karo haitowezekana kwa sababu wazazi wangu hawana huo uwezo wa kugharamia karo hiyo,” alisema kwa sauti iliyokosa matumaini.

Mwanafunzi huyo alisema kuwa lengo lake na ndoto zake ni kusomea kozi ya shahada ya kwanza itakayomwezesha kuhitimu kama daktari mwenye utaalamu wa kutiba matatizo ya meno.

 

View Comments