logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mwanafunzi wa Grade 3 aokolewa baada ya kutekwa nyara na mwalimu wake wa darasa

Juhudi za kumtafuta mwalimu huyo hazikufua dafu.

image
na Davis Ojiambo

Habari10 September 2023 - 14:30

Muhtasari


  • • Wateka nyara walikuwa wameomba fidia ya milioni 10.
  • • Mwanafunzi alitekwa nyara na mwalimu wake wa darasa akishirikiana na washukiwa wengine ambao bado hawajakamatwa.

Mwanafunzi wa miaka 9 wa darasa la tatu kutoka Donholm, Kaunti ya Nairobi aliokolewa baada ya kutekwa nyara na mwalimu wake.

Kulingana na DCI, babake mwanafunzi huyo alikuwa ameenda kumchukua mwanawe shuleni alipompata hayupo.

Aliarifiwa mwanawe ameondoka pamoja na mwalimu wake wa Darasa Erick Mosoti.

Baadaye baba huyo alipokea ombi la fidia ya Sh milioni 10 na kumfanya baba huyo kuripoti katika kituo cha polisi cha Buruburu.

Juhudi za kumtafuta mwalimu huyo hazikufua dafu.

Timu ya wapelelezi kutoka kwa Kamandi ya Mkoa wa Nairobi kwa ushirikiano na wafanyakazi wenza kutoka DCI Buruburu walianzisha operesheni ya kina katika eneo la Kayole Sabasaba.

Operesheni hiyo ilipelekea kuokolewa kwa mtoto huyo ambaye alikuwa amefungiwa katika chumba kinachoaminika kukodiwa na mwalimu mwingine ambaye ni George Odhiambo, anayefanya kazi katika shule moja na mshukiwa mkuu.

Mtoto huyo aliokolewa mara moja na kupelekwa hospitali kuchunguzwa afya yake huku msako ukiendelea.

 

Saa kadhaa baadaye mshukiwa aliyeitwa Fredrick Odhiambo, alipatikana akitoa madai ya fidia badala ya uhuru wa mtoto huyo.

Pikipiki, simu ya mkononi, na vitu vingine vinavyosadikiwa kutumika katika kitendo hicho cha kinyama vilipatikana na kuwekwa kwenye vielelezo huku operesheni ikiendelea kuwaleta washukiwa wengine.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved