In Summary

• Mahakama ilisema kwamba wakati wa kubadilishwa kwa jina, umma haukuhusishwa na kuitaja hatua hiyo kuwa kinyume cha sheria.

Barabara ya Francis Atwoli.
Image: STAR

Mahakama ya Nairobi imetupilia mbali hatua ya barabara ya DikDik jijini Nairobi katika mtaa wa kifahari wa Kilimani kupewa jina la katibu wa muda mrefu katika muungano wa vyama vya wafanyikazi nchini Francis Atwoli.

Barabara hiyo ambayo ilibadilishwa jina kutoka Dik Dik na kuitwa Francis Atwoli ilifanyika hivyo na aliyekuwa gavana wa muda, Ann Kananu lakini mahakama hiyo ilitupilia mbali hatua hiyo kwa kile ilisema kwamba umma haukuhusishwa katika mchakato wa kubadilisha jina la barabara hiyo.

"Uamuzi kama huo ulihitaji ushiriki wa umma kabla ya kufanywa. Michakato kama hii ingetekelezwa bungeni au katika bunge la kaunti ya kaunti ya Nairobi,”

Wakati wa kubadilishwa jina mwaka 2021, kulikuwa na kivangaito kutoka kwa wanaharakati ambao hawakutaka barabara hiyo kubadilishwa jina na kulishuhudiwa kuangushwa kwa bango lenye jina la Atwoli mara kadhaa nyakati za usiku huku uongozi wa kaunti ukirudisha na watu wasiojulikana kuiangusha.

Atwoli alitangaza kuwa serikali ya kaunti ilikuwa imeijenga upya na kuweka CCTV ili kuifuatilia kutoka kwa waharibifu.

Kuchomwa kwa ishara hiyo kulizua hisia tofauti kutoka kwa Wakenya kwenye mitandao ya kijamii huku wengine wakilaani kitendo hicho huku wengine wakiunga mkono uharibifu huo.

Hii si barabara ya kwanza kubadilishwa jina jijini Nairobi kwani itakumbukwa Mwezi Machi mwaka 2021, barabara ya Eastleigh First Avenue ilibadilishwa jina na kuitwa Mohammed Yusuf Haji Avenue kwa heshima ya seneta wa Garissa aliyefariki Februari.

Barabara ya Kapiti Crescent mtaani South B ilibadilishwa jina na kuitwa jina la gwiji wa soka nchini marehemu Joe Kadenge na Accra road kubadilishwa jina na kuitwa aliyekuwa kiongozi wa chama cha Ford Asili Kenneth Matiba (aliyefariki).

 

View Comments