logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Wanawake Meru waapa kuwanyima wanaume tendo la ndoa iwapo Kawira atabanduliwa

“Yule mwanamke ambaye amechaguliwa akiwa MCA ni mmoja tu"

image
na Davis Ojiambo

Habari02 November 2023 - 05:59

Muhtasari


  • • “Sasa ndio maana mimi nimesimama hapa na kusema sisi kama kina mama wa Meru tumekataa kuwashughulikia usiku" walisema.
Wanawake wa Meru.

Wanawake katika kaunti ya Meru wamejitokeza kuonesha kutoridhishwa kwao na hatua ya MCAs wa kaunti hiyo kupitisha mswada wa kumbandua gavana Kawira Mwangaza kwa mara ya pili ndani ya mwaka mmoja.

Wanawake hao ambao waliongea na vyombo vya habari wakati wa maandamano yao ya Amani walidai kwamba jinsia ya kike katika kaunti hiyo imekandamizwa na ile ya kiume.

Walidai kwamba kwa muda mrefu, mwanamke amekuwa akionekana kama mjakazi katika boma ambaye kazi yake ni kupika na kufanikisha tendo la ndoa lakini ikija suala la uongozi wanasukumwa nyuma.

Waliapa kwamba safari hii iwapo seneti itadumisha hoja ya kumbandua Kawira Mwangaza kama gavana, basi watagoma pia kuwapa wanaume wao tendo la ndoa, kuwapikia na pia kuwafulia nguo.

“Yule mwanamke ambaye amechaguliwa akiwa MCA ni mmoja tu. Ndio mjue hapa Meru wanawake tumenyanyazwa na kudhulumiwa kabisa. Wanaume wanatutaka tu tuwafulie nguo, tuwapikie na tuwape tendo la ndoa usiku. Lakini wakati wa uongozi ama wa kula hawatutaki,” alisema mmoja.

“Sasa ndio maana mimi nimesimama hapa na kusema sisi kama kina mama wa Meru tumekataa kuwashughulikia usiku na kuwapikia na kuwafulia nguo kama hawatutaki wakati wa kula, tumekataa hiyo. Watukubali hata sisi wakati wa uongozi, tutawashughulikia na kuwapikia, bora watukubali,” aliongeza huku wenzake wakipitisha ujumbe huo kwa sauti moja.

Wanawake hao walimuomba rais Ruto pamoja na viongozi katika seneti kuangusha hoja hiyo ya kumbandua Kawira Mwangaza, wakisema kwamba imesukumwa na viongozi wanaume ambao hawataki mwanamke kuongoza kaunti yao.

“Tunaomba rais na maseneta, mama wetu [Mwangaza] akifika huko, tafadhali mzingatie kwa kuelewa kwamba Meru wameungana eti hawataki mwanamke kiongozi, wanataka aongoze tu kwa jikoni, kwa kitanda na kwa kufua nguo, hawataki kuona tukiinuka na tumesoma,” alimaliza.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved