In Summary

•Kalonzo alisema kuwa ilibidi Raila Odinga kubadilisha nambari ya simu kwa kuwa ilisambazwa mtandaoni na alipokea jumbe nyingi zikimlazimisha kutafuta nambari mbadala. 

•Makamu huyo wa zamani wa rais aliwataka wakenya kukoma kumdhulumu Raila mitandaoni na kuwataka wawe wakarimu kwa 'baba'

KALONZO MUSYOKA
Image: HISANI

Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka amefichua kuwa kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga amelazimika kubadilisha nambari yake ya simu.

Akizungumza siku ya Alhamisi, Julai 11 katika kongamano la Vijana la Pan African, Kalonzo alisema kuwa nambari ya simu ya waziri mkuu huyo wa zamani ilisambazwa mtandaoni na alipokea jumbe nyingi zikimlazimisha kutafuta nambari mbadala.

“Nilizungumza naye (Raila) nikiwa njiani kuja hapa…. watu walienda kumtembelea jana ikabidi abadilishe namba yake ya simu kwa sababu Gen Z waliweka namba kila mahali,” alisema Kalonzo.

Makamu huyo wa zamani wa rais aliwataka wakenya kukoma kumdhulumu Raila mitandaoni na kumfanyia wema.

"Labda ni kipimo cha uonevu wa mtandaoni tafadhali kuweni wakarimu kwa baba. Iwapo wanaweza kufanya hivyo kwa Raila Odinga, fikiria nani mwingine katika nchi hii hatafanyiwa hivo” Kalonzo aliongeza.

Raila amekuwa akishutumiwa tangu Jumanne, Julai 9 baada ya kukaribisha kuundwa kwa kongamano la sekta mbalimbali kushughulikia masuala yaliyoibuliwa na Gen Z wakati wa maandamano ya hivi majuzi.

Hata hivyo jambo hilo halikuwapendeza vijana wa Gen Z wakidai kuwa wao hawana kiongozi na hawamtambuwi yeyote kama kiongozi wao.

View Comments