Kampuni ya mawasiliano ya Safaricom wamevunja kimya chao baada ya tetesi kuenezwa katika mitandao ya kijamii kwamba wamempa kazi Rodger Magudha, kijana anayezurura mitaani Nairobi na ndege wake aina ya mwewe.
Uvumi huu ulizuka Jumatatu baada ya kijana huyo maarufu kama Nairobi birdman kuonekana katika moja ya duka la Safaricom jijini Nairobi akianya mazungumzo na mhudumu mmoja huku akiwa na ndege wake watatu.
Baadhi katika jukwaa la X walizua tetesi kwamba kijana huyo alikwenda katika duka hilo mahususi kwa ajili ya kuingia kwenye mkataba wa matangazo ya kibiashara na kampuni hiyo kubwa ya mawasiliano humu nchini.
Hata hivyo, Safaricom waimjibu mmoja wa watumizi wa X aliyekuwa akieneza uvumi huo, walisema kuwa si kweli na kufafanua kwamba Nairobi birdman alikwenda tu kama mteja mwingine yeyote kwa huduma kuhusu laini yake ya simu.
“Wacha mzaha, alikuwa katika duka la Safaricom ili ku’replace laini yake na sio kutia saini kandarasi ya matangazo,” Safaricom walisema.
Rodgers Magudha amekuwa gumzo la mitandaoni kaitka kipindi cha wiki za hivi majuzi wengi wakiibua dhana mbalimbali kuhusu uwezo wake wa kupendwa wa ndege hao wa mwituni, kiasi kwamba wanaonekana kupata Amani ya nafsi kwenye mabega yake.
Hata hivyo, kijana huyo alikanusha kutumia dumba kuwavutia ndege hao akisema kuwa ni hali ya asilia tu.