In Summary

• Instagram walieleza kwamba ili kijana wa chini ya miaka 16 kujiunga kwenye Instagram, atahitaji ruhusa ya mzazi.

INSTAGRAM
Image: HISANI

Kampuni ya Meta, imeanzisha akaunti za vijana wa balehe kupitia mtandao wa Instagram, dhumuni likiwa ni kuwalinda watoto dhidi ya maudhui chafu yanayoendelea kwenye mtandao huo wa picha.

Wakitangaza ujio wa akaunti hizo Septemba 17, Instagram walisema akaunti hizo zitaongozwa na wazazi ili kuwazuia wanao dhidi ya kufikia maudhui yasiyowafaa kwenye mtandao huo.

“Leo, tunatanguliza Akaunti za Vijana za Instagram, matumizi mapya kwa vijana, yanayoongozwa na wazazi. Akaunti za Vijana zina ulinzi uliojumuishwa ndani ambao unazuia ni nani anayeweza kuwasiliana nao na maudhui wanayoona,” sehemu ya taarifa kwenye tovuti yao ilisema.

Instagram walieleza kwamba ili kijana wa chini ya miaka 16 kujiunga kwenye Instagram, atahitaji ruhusa ya mzazi.

“Tutawaweka vijana kwenye Akaunti za Vijana kiotomatiki, na vijana walio na umri wa chini ya miaka 16 watahitaji ruhusa ya mzazi ili kubadilisha mojawapo ya mipangilio hii ili kupunguza ukali. Tunajua wazazi wanataka kuwa na uhakika kwamba vijana wao wanaweza kutumia mitandao ya kijamii kuungana na marafiki zao na kuchunguza mambo yanayowavutia, bila kuwa na wasiwasi kuhusu matumizi yasiyo salama au yasiyofaa.”

Meta ilisema kwamba ilitengeneza akaunti hizo wakiwa na fikira za wazazi kwenye vichwa vyao na jinsi ya kuwasaidia kulinda wanao dhidi ya itikadi potovu ambazo huanza kuenezwa kwenye mitandao.

“Tulitengeneza Akaunti za Vijana tukiwafikiria wazazi na vijana. Ulinzi mpya wa Akaunti ya Vijana umeundwa ili kushughulikia matatizo makubwa ya wazazi, ikiwa ni pamoja na wale ambao vijana wao wanazungumza nao mtandaoni, maudhui wanayoona na ikiwa muda wao unatumiwa vizuri,” walisema.

View Comments