In Summary

•Nyamu alisema maneno ya Kuria ni sahihi na kufuatia hayo akalitaka shirika hilo la habari kuweka wazi kazi yake halisi.

•Kuria alidai kuwa shirika la NMG limechukua majukumu ya upinzani na kulitaka lieleze ikiwa bado ni shirika la habari.

Image: INSTAGRAM// KAREN NYAMU

Wakili na seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu mkono mashambulizi ya waziri wa Biashara, Moses Kuria dhidi ya Nation Media Group.

Katika taarifa fupi kwenye mtandao wa Instagram siku ya Jumatatu, seneta huyo wa chama tawala cha UDA alisema maneno ya Kuria ni sahihi na kufuatia hayo akalitaka shirika hilo la habari kuweka wazi kazi yake halisi.

"Moses Kuria yuko sahihi! NMG inafaa kuamua kama ni shirika la habari ama mrengo wa Azimio," Nyamu alisema kwenye Instastori.

Mwanasiasa huyo alinukuu ripoti ya Citizen kuhusu jibu la Muungano wa Wanahabari wa Kenya (KUJ) kwa Waziri Kuria.

KUJ katika taarifa iliyotiwa saini na Katibu Mkuu Eric Oduor siku ya Jumatatu ilisema Kuria "amekuwa ishara ya aibu ya kitaifa" na kulaani matamshi yake mabaya dhidi ya wanahabari wa Nation Media Group.

“Tungependa kumkumbusha Bw Kuria kwamba sasa yeye ni Waziri ambaye matendo na matamshi yake yanafaa kukuza taswira nzuri ya Kenya kama taifa. Sambamba na kanuni za uongozi na sheria ya uadilifu. Maoni yake kwa ripoti za vyombo vya habari kuhusu mojawapo ya kashfa nyingi ambazo zimekumba utawala wa Kenya Kwanza ndani ya muda wa miezi 10 sio tu ni aibu kwa Wakenya, lakini ni uthibitisho kwamba tumbo lake limejaa na anaweza kukunja na hatimaye kutapika kwenye viatu vya njaa. Wakenya bila kuadhibiwa,”  taarifa ilisoma.

“Ingawa tunaunga mkono juhudi zinazoendelea za Naibu Rais Rigathi Gachagua kukabiliana na athari za kukithiri kwa unywaji pombe nchini, ni rai yetu kwamba ili vita hivi vizae matunda, anafaa kutia wavu zaidi ili kuondoa viongozi katika kaunti ambao hawana udhibiti wa idara zao. Ninaweza kumhakikishia Bw Kuria kwamba vyombo vya habari vitaishi maisha marefu kuliko maisha yake ya kisiasa na vitasubiri kwa shangwe kuandika historia yake ya kisiasa,” taarifa hiyo iliongeza.

Mbunge huyo wa zamani wa eneo la Gatundu alizua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumapili baada ya kudaiwa kuchapisha ujumbe wa matusi dhidi ya jumba moja la habari maarufu nchini.

“…. Bado mnaweza kutangaza dalali na matangazo ya mazishi. Hatutazuia hizo,” waziri huyo alisema kwenye Twitter.

Kauli hiyo ilikuja saa chache tu baada ya waziri huyo kuziagiza idara zote ya serikali kususia Nation Media Group.

Wakati akitoa hotuba katika hafla moja katika kaunti ya Embu, mwaniaji huyo wa zamani wa ugavana alidai kuwa shirika hilo la habari limechukua majukumu ya upinzani na kulitaka lieleze ikiwa bado ni shirika la habari.

"Nation Media, muamue kama nyinyi bado ni gazeti ama shirika la habari ama ni chama cha upinzani. Na mimi nimesema, kutoka kesho, kutoka leo sio kesho, idara yote ya serikali nitaona imeweka tangazo kwenye Nation Media, ujihesabu uko nyumbani. Mungu awabariki na awatendee mema," waziri alisema.

Matamshi ya waziri Moses Kuria ya siku ya Jumapili yamezua ghadhabu nyingi kutoka kwa wanamitandao Wakenya.

View Comments