Mwenyekiti wa baraza la magavana Wycliffe Oparanya amesema maambukizi ya covid 19 yamekithiri huku akisema imekuwa vigumu kuwahamisha wagonjwa kutoka kaunti moja hadi nyingine .
Akizungumza wakati wa kongamano la sita kuhusu corona kati ya serikali kuu na za kaunti katika Ikulu ya Nairobi Oparanya amesema amesema panafaa kurejeshwa masharti yote ya kupambana na ugonjwa huo.
Oparanya amesema kumekuwa na utepetevu katika kutekeleza kanuni hizo hasa katika maeneo ya burudani ,sekta ya uchukuzi na masoko .
" Viongozi wa kisiasa wamekuwa wasambazaji wakubwa wa virusi hivi . Hatua hiyo imesababisha kuongezeka kwa visa vya mambukizi na kufeli kwa juhudi za kuwapata wote waliotangamana na watu walioambukizwa’ Oparanya amesema
Mwenyekiti huyo wa baraza la magavana alimtaka rais kurejesha muda wa kafyu kuanzia saa tatu usiku hadi saa kumi alfajiri kwa angalau mwezi mmoja kutoka kipindi cha sasa cha saa tano usiku hadi saa kumi na moja .
Serikali za kaunti zitaanzisha kampeini ya #NoMaskNoService ambapo wasiokuwa na barakoa hawatopewa huduma katika kaunti ili kuhakikisha kwamna wananchi wanavalia maski ili kujikinga dhidi ya ugonjwa huo
Oparanya amesema kuongezeka kwa visa vya maambukizi kumefanya vigumu kwa kaunti kuwalaza wagonjwa Zaidi .
" Kwa kweli ni mgogoro mkubwa .wagonjwa wengi wanapoteza maisha yao wakisafirishwa kwenda Nairobi ili kupata matibabu’ amesema
Ameongeza kwamba kaunti 12 hazina vitanda 300 kama inavyohitajika ilhali kaunti 11 vina chini ya vitanda 5 vya ICU.` Kuna uwezekano wa rais Uhuru Kenyatta kufunga baadhi ya sehemu za nchi au kuongeza muda wa kafyu wakati atakapokutana na baraza la usalama wa kitaifa baadaye wiki hii