Rais Uhuru Kenyatta amezihimiza  pande zinazohusika katika mzozo unaoendelea nchini Ethiopia kutafuta njia ya amani ya kukomesha mzozo huo.

Rais alitahadharisha dhidi ya kuzuka kwa vita kamili nchini humo akisema kwa muda mrefu Kenya na Ethiopia zimekuwa nguzo za amani na  uthabiti katika kanda hii.

Aliihimiza Serikali ya Kitaifa na kundi la wapiganaji wa Tigrayan People's Liberation Front (TPLF) kupunguza uhasama akisema mgogoro huo unatishia kuharibu mafanikio yaliyoafikiwa na raia wa  Ethiopia katika kustawisha nchi yao.

Rais alisema hayo siku ya Jumatatu jioni katika Ikulu ya Nairobi wakati wa mkutano na   Naibu Waziri Mkuu wa  Ethiopia  aliye pia  Waziri wa Mashauri ya Nchi za Kigeni Demeke Mekonnen ambaye alimtembelea.

Naibu wa Waziri Mkuu wa Ethiopia pia alimkabidhi Rais Kenyatta risala maalumu kutoka kwa Waziri Mkuu Abiy Ahmed na kumuarifu Kiongozi wa Nchi kuhusu hali ya kisiasa na usalama nchini Ethiopia.

Huku akitambua juhudi za ndani zinazofanywa kukomesha mzozo huo, Rais Kenyatta alihimiza pande zinazozozana kutilia manani mahitaji ya  kibinadamu ya raia wao kwa kufungua barabara kwa ajili ya usafirishaji wa bidhaa muhimu. 

Wengine waliokuweko katika mkutano huo ni Waziri wa Mashauri ya Nchi za Kigeni Raychelle Omamo, Mshirikishi wa Wizara hiyo Ababu Namwamba na Mkuu wa Utumishi wa Umma Dkt Joseph Kinyua.

Ujumbe huo wa  Ethiopia ulijumuisha Katibu katika Wizara ya Mashauri ya Nchi za Kigeni Woineshet Tadesse na Balozi wa nchi hiyo hapa Kenya Meles Alem.

 

View Comments