Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga wakizindua zoezi la ukusanyaji saini kufanikisha ripoti ya BBI. (Picha: PSU)

Shughuli ya ukusanyaji saini ili kufanikisha mageuzi yanayopendekezwa katika ripoti ya BBI ilizinduliwa rasmi siku ya Jumatano.

Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga waliongoza hafla hiyo.

Rais Uhuru Kenyatta amewajibu wanaokosoa mchakato wa BBI akisema kwamba mwafaka wake na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ulileta amani nchini Kenya.

 
 

“Tunasahau haraka sana kwa sababu ya amani tumekuwa nayo kwa miaka miwili, watu wengine wanaona ni kawaida”.

Rais Uhuru Kenyatta atia saini wakati wa hafla ya kuzindua saini za kufanikisha ripoti ya BBI. (Picha PSU)
Rais Kenyatta alisema kwamba kulingana na taarifa za ujasusi alizokuwa akipokea akiwa rais, Kenya ingesambaratika kama yeye na Raila hawangekubali kuunganisha taifa.

Kiongozi wa taifa alisema kwamba hii haikuwa mara ya kwanza yeye kuungana na mpinzani wake kwa lengo la kuunganisha taifa na kuleta amani. Alisema alifanya hivyo na naibu rais William Ruto katika hatua iliyopunguza joto la kisiasa nchini.

“Hii si mara mara yangu kwanza kufana hivi, hata mwenzangu Deputy wangu nilireach out kwake, sasa wenzangu kuna mambo gani mabaya nikiendea ndungu yangu Raila ili tuunganishe taifa.

Makatibu wa kamati maalum inayosimamia zoezi la ukusanyaji wa saini za BBI mbunge wa  zamani Dennis Waweru na mbunge wa Suna East Junet Mohamed walisema kwamba shughuli ya ukusanyaji saini inatarajiwa kuchukuwa muda wa wiki moja kukamilika.

“Tunatoa wito kwa wakenya wenye nia njema, wale wanaotaka kuangamiza ufisadi, ukabila, vitisho, kutengwa kwa baadhi ya maeneo, kuimarisha Maisha ya vijana, wanawake na walemavu kuabiri gari la BBI,” Waweru alisema siku ya Jumatatuu.

Kulingana na kamati inayoongozwa na Waweru na Junet, shughuli ya kukusanya saini milioni moja kutoka kaunti zote 47 itachukuwa tu siku saba.

 

Wawili hao walitoa hakikisho kwamba zoezi hilo litafanyika kuambatana na kanuni na masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya Covid-19.

View Comments