In Summary

• Kamati ya bunge ya  afya inataka serikali kutoa shilingi milioni 500 kutoka kwa hazina ya kitaifa.

• Mwenyekiti Sabina Chege pia anataka serikali kuwapa wahudumu vifaa vya kujikinga katika mabohari ya kemsa.

Wahudumu wa afya. (Picha Maktaba)

Wahudumu wa afya watapewa bima ya afya ya jumla ili wapate huduma za matibabu wanapoambukizwa na virusi vya covid-19 ikiwa pendekezo la kamati ya afya ya bunge litaadhinishwa na bunge na kutekelezwa na serikali.

Kamati ya bunge ya  afya inataka serikali kutoa shilingi milioni 500 kutoka kwa hazina ya kitaifa ili kuwapa wahudumu wote wa afya bima ya matibabu dhidi ya maambukizi ya Covid-19.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Sabina Chege siku ya Alhamisi alisema kwamba ni jambo la kusikitasha kuona wahudumu wa afya wanaohatarisha maisha yao kuokoa maisha ya walioambukizwa virusi vya korona wenyewe hawana bima kugharamia matibabu yao wanapoambukizwa virusi hivyo.

Miungano ya wahudumu wa afya nchini ilikerwa na tangazao la waziri wa Afya Mutahi Kagwe kwamba hazina ya bima ya kitaifa ya matibabu NHIF haitaweza kuendelea kugharamia matibabu ya Covid-19.

Katibu mkuu wa KMPDU Chibanzi Mwachonda alikuwa ametangaza kwamba madaktari watagoma ikiwa maslahi yao hayatazingatiwa na kupewa kipao mbele. Hii ilikuwa baada ya madaktari kadhaa wenye tajiriba kuaga dunia kutokana na Covid-19.

Wizira ya afya hata hivyo baadaye ilisema kwamba mazungumzo yalikuwa yanaendelea ili bima ya NHIF ianze kutoa bima ya jumla ya matibau kwa wahudumu wa afya ili waendelee kuhudumia wananchi.

Mwenyekiti wa kamati ya afya Sabina Chege pia alisema kwamba kamati yake inataka serikali kutoa vifaa vyote vya kujikinga katika mabohari ya mamlaka ya usambazaji wa bidhaa za matibabu nchini (KEMSA) kutumika na wahudumu wa afya ambao wanahatarisha maisha yao kuhudumia wakenya.

Kamati hiyo pia iliagiza hospitali zote za umma kutowatoza wakenya ada za bidhaa za kujikinga wanapolazwa kutokana na maambukizi ya virusi vya korona.

View Comments