In Summary

• Magenge ya Confirm na WaTZ yamekuwa yakihangaisha wenyeji.

• Polisi wamethibitisha vifo vya watu watatu.

• Polisi wanashika doria. 

crime scene

Wakaazi wa Nakuru wanaishi kwa hofu baada ya watu watatu kuuawa kwa kukatwa na panga katika mtaa wa Kivumbini mjini Nakuru.

Wenyeji wanasema kwamba vijana waliokuwa kwa pikipiki walivamia wakaazi wasiokuwa na hatia na kuwashambulia kwa panga na visu.

Wanadai kwamba kuna magenge mawili ya uhalifu ambayo yamekuwa yakiwahangaisha kwa muda mrefu sasa.

Wanasema makundi hayo mawili yanafahamika  kama Confirm na WaTZ na yamekuwa yakitekeleza uhalifu mjini humo.

Jamaa mmoja wa waliofariki katika uvamizi wa jana mwendo wa saa tisa alasiri alisema kwamba makundi hayo sasa yamekuwa yakikabiliana kuonyesha ubabe wao na huenda uvamizi wa jana ulikuwa wa kulipiza kisasi.

Mwanamume mmoja aliyekuwa mlemavu alikatwa na kudungwa visu hadi kufa na wanachama wa genge moja baada ya kushindwa kukimbia kama wenzake.

“Vijana wawili walikuja wakiwa kwa pikipiki na kuanza kushambulia watu kwa mapanga na vifu, wengi walifanikiwa kutoroka lakini huyu kijana ni mlemavu na ana mguu mmoja alishindwa kukimbia na wakamkata kata kwa mapanga na kumdunga visu,” mkaazi mmoja alisema.

Kamishna wa kaunti ya Nakuru Erastus Mbui alithibitisha tukio hilo na kusema kwamba watu watatu waliuawa.

Alisema kwamba usalama umeimarishwa na polisi wanaendelea kushika doria. Mbui aliwahakikishia wenyeji kwamba wahusika wote watakabiliwa vilivyo.

Alitowa wito kwa wakaazi kushirikiana na maafisa wa usalama kuwatambua wahalifu.

View Comments