Naibu wa rais William Ruto amewaonya wafanyikazi wa umma dhidi ya kutumiwa vibaya na wanasiasa kwa kukiuka sheria kupitia utumizi mbaya wa maamlaka na afisi zao .
Akizungumza huko Nakuru wakati wa mazishi ya mamake mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri ,Ruto amesema wanaolenga kuvuruga mshikimano wa kijamii uliopo sasa wana hila .
Amesema wafanyikazi wanaokubali kutumiwa na wanasiasa wanatishia kulirejesha taifa katika kipindi kibaya cha ukabila .
“ Badala ya kukabiliana na uhalifu ulipo sasa nchini ,wanataka kuwachochea wananchi kuendeleza ukabila’ amesema Ruto .
Aliongeza kusema ‘ Nataka kuongeza kwamba kutumia mfumo wa idara za uchunguzi na mashtaka kuwakandamiza watu wa kabila Fulani au mrengo fulani wa kisiasa ni jambo baya’
Amesema kuna watu walionufaika pakubwa na siasa za uhasama na ukabila na wamegundua kwamba hawana manufaa ya kupata wakati pana amani nchini .
“ Wanajaribu kuwatumia watumishi wa umma kuvuruga Amani miongoni mwa wakaazi wa Rift Valley … wafanyikazi wa umma wamecha kazi zao na sasa wanapiga siasa ..wanafanya kazi ya shetani na nataka kuwaambia kwamba hawatafaulu ..’
Ruto amewaambia wafanyikazi wa umma walio na jukumu la kuwalinda wananchi kutotumia nafasi zao kufanya mabaya kwani hatua hiyo itakuwa hatari kwa nchi .