In Summary

•Mkutano kati ya wawakilishi wa Jubilee na wa ODM ulifanyika siku ya Alhamisi katika hoteli ya Nairobi ambapo mazungumzo kuhusiana na kuundwa  kwa muungano  yalianza rasmi.

•Tuju alieleza kuwa chama cha Jubilee kitakaribisha vyama vingine ambavyo vitaonyesha nia.

Wawakilishi wa vyama vya ODM na Jubilee wakiwa kwenye mkutano katika hoteli ya Nairobi
Image: Hisani

Chama cha Jubilee kinashirikiana na kile cha ODM kuunda muungano mmoja thabiti tunapokaribia uchaguzi mkuu wa 2022.

Akizungumza na wanahabari siku ya Ijumaa, katibu mkuu wa chama cha Jubilee, Raphael Tuju alifichua kuwa vyama hivyo viwili vimekuwa vikishiriki mazungumzo ili kufanikisha muungano na kuteua mgombeaji mmoja wa kiti cha urais.

"Tumekuwa tukishiriki mazungumzo na wenzetu wa ODM. Iwapo tutakuwa na maafikiano kuhusiana na kuunda muungano,basi tutateua mgombeaji mmoja kuwania kiti cha urais" Tuju alisema

Tuju alieleza kuwa chama cha Jubilee kitakaribisha vyama vingine ambavyo vitaonyesha nia.

Tayari chama cha KANU  kinachoongozwa na seneta wa Baringo, Gideon Moi, kimekubali kushirikishwa huku chama cha Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka kikionyesha nia yake.

"Ni sharti uwe muungano wa wale wenye nia. Kama kunavyo vyama vingine ambavyo vina nia basi tutavishirikisha" Tuju alisema.

Mkutano kati ya wawakilishi wa Jubilee na wa ODM ulifanyika siku ya Alhamisi katika hoteli ya Nairobi ambapo mazungumzo kuhusiana na kuundwa  kwa muungano  yalianza rasmi.

Kati ya waliohudhuria ni pamoja na katibu mkuu wa Jubilee Raphael Tuju,  Edwin Sifuna wa ODM, mwenyekiti wa ODM John Mbadi, na naibu mwenyekiti wa Jubilee David Murathe.

Iwapo makubaliano yataafikiwa, muungano huo utasajiliwa na msajili wa  vyama vya kisiasa nchini kwenye hafla itakayohudhuriwa na rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga.

View Comments