In Summary

• Hatua ya kuhusisha vikosi zaidi vya polisi kumsaka mshukiwa ilitokana na tukio la pili ambapo afisa huyo anashukiwa kumpiga risasi tena mtu mwingine eno la Juja,

• Wapelelezi wamebaini kuwa alimshawishi mwanamume huyo waende chumbani baada ya kulipia, kabla ya kumpiga risasi kichwani kwa karibu.

Mshukiwa wa mauji ya watu wawili Caroline Kangogo
Image: HISANI

Maafisa wa DCI wanamsaka afisa wa polisi wa kike ambaye anaonekana kuwa kwenye msururu wa mauaji.

Vitengo kadhaa vya polisi vimewekwa katika hali ya tahadhari kumsaka afisa wa polisi Caroline Kangogo, mtuhumiwa wa mauaji ya Konstebo wa Polisi John Ogweno, huko Nakuru.

Hatua ya kuhusisha vikosi zaidi vya polisi kumsaka mshukiwa ilitokana na tukio la pili ambapo afisa huyo anashukiwa kumpiga risasi tena mtu mwingine eno la Juja, karibu kilomita 200 kutoka tukio la kwanza. Jamaa aliyeuawa alitambuliwa kama Peter Ndwiga Njiru, 32.

Afisa huyo ambaye alitajwa kama mtu aliyejihami na hatari na idara ya polisi alichukua bastola ya mhasiriwa wa kwanza Ogweno, bastola ya Ceska iliyokuwa na risasi, alimshawishi Njiru kwenda Hoteli ya Dedamax mtaani Kimbo, Juja mwendo wa saa nne usiku wa Jumatatu, mashahidi walisema.

Baadaye aliibuka kutoka kwenye chumba usiku wa manane Jumatatu na kutorokea sehemu isiyojulikana, akiacha mwili wa mtu waliyekuwa naye chumbani.

Wapelelezi wamebaini kuwa alimshawishi mwanamume huyo waende chumbani baada ya kulipia, kabla ya kumpiga risasi kichwani kwa karibu.

Haijulikani ni nini kilichochea mauaji ya mtu wa pili.

Kangogo baadaye alimwambia mhudumu anayefanya kazi katika eneo alimokuwa amekodisha chumba cha kulala kwamba alikuwa anaenda kununua dawa ya meno, kabla ya kutoroka.

Mkurugenzi wa DCI George Kinoti alisema mshukiwa ambaye ana silaha na hatari amekuwa akikimbia tangu mapema Jumatatu asubuhi, baada ya kumuua Ogweno, ambaye alikuwa akihudumu kama afisa wa polisi mjini Nakuru.

"Tunaonya umma haswa wanaume kuwa macho na afisa huyo mwovu, ambaye anawashawishi wanaume kwa mtego wake kabla ya kuwaua kinyama," alisema.

“Mtu yeyote asimwamini kwani ana silaha na ni hatari. Ukimwona mtuhumiwa anayejifunika kwenye buibui, usisite kuwasiliana nasi kupitia simu yetu ya bila malipo ya 0800722203. ”

Maafisa wa polisi wakiongozwa na OCS wa Nakuru walitembelea eneo la tukio na kuthibitisha kwamba afisa huyo alikuwa ameaga dunia.

Wanashuku kuwa alipigwa risasi upande wa kulia wa kichwa na akatokwa na damu hadi kufa.

Jiwe lililotumiwa kuvunja dirisha la gari na chuma pia vilipatikana na vitatumika katika ushahidi.

Maafisa wanashuku kuwa huenda mauji haya yamechochewa na mzozo wa kimapenzi.

View Comments