In Summary

•Kuria amekuwa hospitalini tangu mwishoni mwa mwezi Septemba baada ya kuugua maradhi ambayo hayajathibitishwa

•Licha ya tofauti zao za kisiasa, kinara wa ODM Raila Odinga alichukua hatua ya kumtembelea Kuria hospitalini siku ya Jumanne.

Image: FACEBOOK// MOSES KURIA

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria amekuwa hospitalini tangu mwishoni mwa mwezi Septemba baada ya kuugua maradhi ambayo hayajathibitishwa.

Mwanasiasa huyo ambaye amejitambulisha kama mmoja wa wakosoaji wakubwa wa rais Uhuru Kenyatta amelazwa katika hospitali moja jijini Nairobi ambako anaendelea kupokea matibabu.

Katika juhudi za kurejesha afueni yake, mbunge huyo alifanyiwa upasuaji asubuhi ya Jumatano.

"Mungu ni mwenye huruma. Nimetoka thieta vizuri! Tunasifu jina lake" Kuria alitangaza kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Katika kipindi ambacho mbunge huyo amekuwa hospitalini amepokea msururu wa wageni ambao wamekuwa wakienda kumuuguza pole na kumtakia afueni ya haraka.

Wanasiasa wenzake na watu wakuu serikali ni miongoni mwa wageni ambao Kuria amepokea katika kipindi hicho.

Licha ya tofauti zao za kisiasa, kinara wa ODM Raila Odinga alichukua hatua ya kumtembelea Kuria hospitalini siku ya Jumanne.

Raila alikuwa ameandamana na mbunge wa Mbeere Kusini Geoffrey Kingangi, mbunge wa Githunguri Gabriel Kago, mbunge wa EALA Mpuru Aburi  kati ya viongozi wengine.

Awali siku hiyo kinara wa ANC Musalia Mudavadi alikuwa ameandamana na viongozi wengine kumtakia afueni ya haraka mbunge huyo.

Naibu rais William Ruto alikuwa miongoni mwa wageni wa kwanza kumtembelea mwandani wake Kuria.  Ruto aliandamana na mbunge wa Mumias Mashariki Ben Washiali na  Philip Koech.

Kiongozi wa Wiper Stephen Kalonzo Musyoka na mbunge wa zamani Martha Karua pia walimtembelea mbunge huyo wa muhula wa pili mnamo Septemba 27. 

Spika wa bunge la kitaifa Justin Muturi, gavana wa Nakuru Lee Kinyajui, seneta wa Baringo Gideon Moi, mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua, mbunge wa zamani Cyrus Jirongo na mwenyekiti wa NYS Njuki Mwaniki walifika hospitalini kumtakia afueni ya haraka Moses Kuria mapema wiki hii.

Kuria amewashukuru wote ambao wameenda kushirikiana naye katika ssafari yake ya matibabu.

View Comments