In Summary

• Wanjala ambaye alikuwa ametoroka seli za polisi alipokuwa anasubiri kufikishwa mahakamani alikuwa amefanikiwa kusafiri kutoka Nairobi hadi Bungoma alipotambuliwa na wananchi siku ya Alhamisi jioni.

Mshukiwa Masten Milimu Wanjala
Image: DCI

Jamaa aliyekiri kuua watoto 13 katika maeneo mbali mbali nchini Kenya Masten Wanjala ameuawa na umati wa watu katika Kijiji cha Mukhweya eneo bunge la Kabuchai kaunti ya Bungoma.

Wanjala ambaye alikuwa ametoroka seli za polisi alipokuwa anasubiri kufikishwa mahakamani siku ya Jumatano kujibu mashtaka ya mauaji na alikuwa amefanikiwa kusafiri kutoka Nairobi hadi Bungoma alipotambuliwa na wananchi siku ya Alhamisi jioni.

Kulingana na Chifu wa eneo hilo wananchi walimtambua Wanjala na kuanza kumshambulia.

Wanjala mwenye umri wa miaka 25 alikuwa ametoroka seli za Polisi katika kituo cha polisi cha Jogoo road mjini Nairobi siku ambayo alitarajiwa kupelekwa mahakamani kwa mauaji ya watoto kadhaa.

Alishangaza wengi alipokiri kuua zaidi ya watoto 10 na hata kuelekeza maafisa wa polisi hadi mahali alikokuwa ametupa miili ya angalau watoto wanne, na miili ambayo ilikuwa tayari imeanza kuharibika kupatikana.

Alikuwa ameonyesha maafisa wa upelelezi kitabu ambamo alikuwa amenakili majina ya watoto aliokuwa ameua.

Polisi watatu waliokuwa wakishika doria siku ambayo alitoroka tayari wamesimamishwa kazi na kukamatwa kwa madai ya kumsaidia kutoroka pamoja na utepetevu kazini.

Walifikishwa mahakamani siku ya Alhamisi.

Idara ya polisi ilikuwa imetangaza msako mkali kumtafuta jamaa huyo.

Bado haijulikani vile mshukiwa wa makosa ya mauaji ya watu wengi alifanikiwa kutoroka seli za polisi licha ya ulinzi mkali na hata kufanikiwa kusafiri kutoka Nairobi hadi kaunti ya Bungoma alikokutana na mauti yake.

Kifo chake ni afueni kwa wananchi ambao walikuwa wameelezea hofu kuhusu maisha yao walipopata taarifa za kutoroka kwake kutoka seli za polisi.

View Comments