In Summary

• Wanjala kabla ya kuuawa alisema kwamba alijifanya mmoja wa washukiwa wa makosa madogo na kuwahonga maafisa waliokuwa wakishika doria kwa pesa alizokuwa nazo na kuruhusiwa kwenda  Jumanne usiku.

Image: DCI

Masten Wanjala aliyekiri kuua kinyama watoto kadhaa siku ya Alhamisi alisimulia jinsi alitoroka seli ya polisi kabla ya kuuawa Bungoma.

Wanjala aliwaambia wananchi waliomuua baadaye kwamba alijifanya kuwa mmoja wa washukiwa wa makosa madogo na kuwahonga maafisa waliokuwa wakishika doria kwa pesa alizokuwa nazo na kuruhusiwa kwenda  Jumanne usiku.

Polisi ambao walizungumza na umati huo walisema Wanjala kisha alipata lifti kwenye lori la kwenda Bungoma ambapo alijiunga na wanakijiji.

"Hata hivyo hakujua hawakumtaka huko," polisi walisema.

Wanjala ambaye alikuwa kwenye seli kwa karibu mwezi mzima alitoroka baada ya polisi kuwakamata makumi ya washukiwa kwa kukiuka kanuni za kudhibiti maambukizi ya Covid-19 na kuwachanganya na wale ambao walikuwa chini ya ulinzi.

Ilichukuwa hadi Jumatano asubuhi ambapo maafisa ambao walikuwa wakichukua doria walipogundua kuwa mshukiwa wa mauaji ya zaidi ya watu 10 Masten Wanjala alikuwa ametoroka.

Wanjala, 25, alitoroka kutoka kwa seli za kituo cha polisi cha Jogoo wakati washukiwa wengine walikuwa wakitengwa kutoka kwa raia wengine.

Aliongoza polisi hadi maeneo mbali mbali alikokuwa ameficha miili ya wahasiriwa wake na kuigiza vile alitekeleza mauaji yao, akarekodi sauti na akaonyesha wachunguzi kitabu chake kilichoelezea mauaji hayo.

Mara nyingi alijifanya kama mkufunzi wa mpira wa kandanda.

Alitarajiwa kortini kwa kutajwa kwa kesi kadhaa zilizo chini ya uchunguzi.

Wahasiriwa wake wote isipokuwa mmoja walikuwa wavulana na wengi walikuwa wamepewa dawa za kulevya, kisha kunyongwa.

Wanjala aliwaambia polisi wakati mwingine kwamba aliinywa damu ya baadhi ya wahasiriwa wake.

View Comments