In Summary

•Walisema  kwamba  tayari walikuwa wamejaza na kurudisha fomu za P3  kuhusiana na shambulio hilo na wanatarajia polisi watachukua hatua.

•Stephanie alidai kwamba alinyongwa na pacha mmoja huku akieleza kuwa kwa sasa hawezi kumeza chakula vizuri ilhali dadake alisema kwamba aliugua majeraha kwenye mkono wake kufuatia kichapo alichopokea.

•Walidai kwamba mapacha wale waliwatishia kuwapiga risasi wakati wa tukio lile

Stephanie, Cheryl na mjomba wao Philip Murgor wakihutubia wanahabari
Image: CYRUS OMBATI

Dada wawili ambao wanadai kushambuliwa na mapacha wawili Edward Ndichu na Paul Ndichu  wamejitokeza kusimulia drama ambayo ilisababisha vurugu katika hoteli ya Ole Sereni siku ya Jumamosi.

Stephanie na Cheryl Murgor walizungumza wakiwa wameandamana na wakili Phili Murgor ambaye ni mjomba wao na wakaomba hatua ichukuliwe dhidi ya ndugu wale kufuatia tukio ambalo lilirekodiwa kwa camera.

Stephanie alidai kwamba alinyongwa na pacha mmoja huku akieleza kuwa kwa sasa hawezi kumeza chakula vizuri ilhali dadake alisema kwamba aliugua majeraha kwenye mkono wake kufuatia kichapo alichopokea.

" Tunatarajia haki. Ingawa Inspekta Jenerali wa polisi ametupatia hakikisho kwamba tukio hilo litachunguzwa kikamilifu, kwetu kulingana na ushawishi mkubwa na nguvu za wa wahusika, tunaagiza Inspekta Jenerali akabidhi uchunguzi kwa timu ya maafisa kutoka makao makuu ambao watahakikisha kwamba uchunguzi umekamilishwa haraka iwezekanavyo na kupitishwa kwa ODPP ili mapacha wa Ndichu waweze kushtakiwa" Dada wale walisema.

Walisema  kwamba  tayari walikuwa wamejaza na kurudisha fomu za P3  kuhusiana na shambulio hilo na wanatarajia polisi watachukua hatua.

Wahasiriwa hao wawili hufanya biashara ya kuuza nguo jijini Nairobi.

Walisema kwamba walilkuwa wanahudhuria sherehe ya baada ya harusi katika ghorofa la 10 la hoteli ya Ole Sereni wakiwa wameandamana na marafiki wao wawili Samuel Ramdas na Patrick Koech.

Inadaiwa kwamba mwendo wa saa nane unusu usiku, mmoja wa mapacha wale alimpita Stephanie vibaya na mwanadada huyo akamwambia kuwa anamfahamu kama mume wa Janet Mbugua.

Mwanadada ambaye alikuwa ameandamana na mapacha wale akasema kwa sauti kwamba pacha yule alikuwa mume wa Janet Kitambo.

Wakati Stephanie alikuwa anaenda kutoka, mmoja wa ndugu wale alimtusi.

" Ghafla ndugu mmoja ambaye alikuwa amevaa nguo nyeusi akamrukia Stephanie na kuanza kumnyonga kwenye koo. Wakati mpenzi wake alijaribu kumuokoa akashikwa kwenye koo pia.Baada ya hatua chache aliwaachilia wapenzi hao wawili lakini akaendelea kuwapa vitisho kwamba alikuwa ametambua sura zao" Wakili Murgor alisema.

Makabiliano mengine yalitokea wakati dada wale wawili walikuwa wanaelekea kwa gari lao.

"Ghafla mapacha wale wawili wakajitokeza kwenye ghorofa ya chini wakiwa wameandamana na rafiki yao mwanamke na wakaendelea kumshambulia Cheryl na Patrick  na baadae ndugu hao wawili wakaenda kwenye kiingilio cha mbele ambapo Stephanie na Samuel walikuwa wamesubiri" Alisimulia Murgor.

Inadaiwa kwamba ndugu mmoja alivunja kioo cha  upande wa kulia huku ndugu mwingine akivunja cha upande wa kushoto kabla ya kurudi ndani kushambulia Cheryl.

"Wakati wa tukio, ndugu hao walitishia kupiga wahasiriwa risasi" Murgor alisema.

Baadae ndugu wale waliomba kuwalipa shilingi 110, 000 kama fidia ya hasara ya kuharibiwa kwa gari lao, malipo ambayo walifanya kutumia Mpesa. Hata hivyo baada ya hapo ndugu wale waliagiza pesa zile zirejeshwe.

Kulingana na Murgor, Wanadada wale hawakukubali kulipwa kama fidia ya kushambuliwa na kusababishiwa majeraha mwilini.

Mwanamke ambaye alikuwa ameandamana na mapacha wale alipiga ripoti akidai kwamba madai ya Murgor yalikuwa ya uongo.

Bi Munira Hassan alidai kwamba alishambuliwa na dada wale wawili na akatoa ripoti ya hospitali iliyoonyesha kuwa alikuwa na majeraha.

Alisema kwamba mapacha wale wawili walikuwa wanajaribu kumnusuru kutoka kwa kichapo ambacho alipewa na dada wale na wapenzi wao.

"Nywele zangu zilivutwa.. nilipoteza fahamu kwa sekunde kadhaa na nikipata majeraha kwenye mwili na sehemu ya mbele ya kichwa kama ilivyoonyeshwa kwenye ripoti ya daktari" Alisema.

Alihimiza dada wale wasubiri uchunguzi wa polisi ukamilike kuhusiana na tukio hilo. 

(Utafsiri: Samuel Maina)

View Comments