In Summary

• Moraa alisema kwamba mamake alikuwa mgonjwa na mdhaifu na yeye ndiye alikuwa anamsaidia kazi za pale nyumbani.

•Alidai kwamba mama yake alikuwa ametoa tahadhari kuhusiana na kipande cha ardhi ambacho mwalimu mmoja alitaka kunyakua bila kukamilisha malipo ambayo walikuwa wamekubaliana.

Janet Moraa, Binti ya marehemu Jemimah Nyang'ate ambaye ni mmoja wa wakongwe waliouawa Kisii kufuatia madai ya Uchawi akihutubia wanahabari siku ya Alhamisi
Image: WILFRED NYANGARESI

Janet Moraa ambaye ni binti wa Jemimah Nyangate, mmoja wa wakongwe wanne waliouawa Kisii kufuatia tuhuma za kujihusisha na uchawi amesema kwamba mauaji ya mamake yalitokana na mgogoro wa shamba ila sio uchawi kama ilivyodaiwa.

Marehemu Nyang'ate alikuwa miongoni mwa wakongwe wanne ambao waliuawa na wanakijiji katika eneo la Nyagonyi siku ya Jumapili baada ya kushukiwa kuteka nyara mwanafunzi wa shule ya upili usiku.

Alipokuwa anahutubia wanahabari katika hoteli ya Mayfair jijini Nairobi siku ya Alhamisi, Moraa ambaye alikuwa ameandamana na wanaharakati  na baadhi ya viongozi wanawake kutoka eneo la Gusii alisema kwamba mamake alikuwa mgonjwa na mdhaifu na yeye ndiye alikuwa anamsaidia pale nyumbani.

Alieleza kwamba marehemu alikuwa amepewa ruhusa kutoka hospitali siku ya Jumamosi kabla ya wakazi kufika nyumbani kwao na kumchukua mamaye asubuhi iliyofuata wakidai kwamba kijana aliyekuwa ametekwa nyara alimtambua kama mmoja wa wachawi waliotekeleza kitendo kile.

Moraa alisema kwamba siku tatu baada ya mama yake kuuawa, wakazi walirudi pale nyumbani kwao na kutoa kila kitu nje kabla ya kuteketeza nyumba yote.

Alidai kwamba mama yake alikuwa ametoa tahadhari kuhusiana na kipande cha ardhi ambacho mwalimu mmoja alitaka kunyakua bila kukamilisha malipo ambayo walikuwa wamekubaliana.

Alisema kwamba familia yao itaweza kupata amani pindi tu mwalimu yule atakapotoka kwa shamba lao.

Wengine ambao waliuawa pamoja na Bi Nyang'ate ni pamoja na Agnes Ototo 57, Sigara Onkware 62 na Sindege Mayaka 85.

Kufikia jioni ya Jumatatu washukiwa wanne walikuwa wametiwa mbaroni tayari huku wengine 11 wakiendelea kusakwa katika vijiji mbalimbali vya eneo la Kitutu Chache.

(Utafsiri: Samuel Maina)

View Comments