In Summary

• Alisema washindani wake bado walikuwa wamejificha nyuma ya Rais Uhuru Kenyatta 'labda wakisubiri ridhaa'.

Naibu Rais William Ruto amesema hakuna mshindani wake aliyekuwa tayari kukabiliana naye kwa sababu hawakuwa na ajenda za nchi.

Alisema washindani wake bado walikuwa wamejificha nyuma ya Rais Uhuru Kenyatta 'labda wakisubiri ridhaa'.

Akizungumza katika vituo mbalimbali vikiwemo Naitiri, Kamukuywa, Ndivisi, Matisi, Nalondo, Angurai na Kamolo katika ziara yake ya kuwezesha Kaunti za Bungoma na Busia mnamo Alhamisi, Dkt Ruto aliwaambia washindani wake kuibua ajenda zao na kukabiliana naye.

"Washindani wangu bado wamejificha nyuma ya Rais Uhuru Kenyatta kwa sababu na hawako tayari kunikabili kwa sababu hawana ajenda yoyote kwa Wakenya," Dkt Ruto alisema.

Aliongeza: "Ikiwa wana nia ya dhati, wakome kutafuta msaada kutoka kwa Rais Kenyatta na wamkabili. Wanafaa kumruhusu Rais kutekeleza miradi yake ya urithi badala ya kumsumbua."

Aliandamana na wabunge Benjamin Washiali (Mumias Mashariki), Didmus Barasa (Kimilili), Dan Wanyama (Webuye Magharibi), Fred Kapondi (Mt Elgon), Mwambu Mabonga (Bumula) na John Waluke (Sirisia).

Ruto alishangaa kwa nini washindani wake walikuwa na shughuli nyingi kukosoa mtindo wa uchumi wa UDA wa Bottom up badala ya kuja na zao.

"Hakuna haja ya washindani wangu kukosoa mtindo wetu wa uchumi wa Bottom up ambao unalenga kuwawezesha wananchi wengi wa kawaida. Wanafaa kuibua ajenda zao," alisema.

Wakati huo huo, Naibu Rais, alisema ni wakati wa kukomesha siasa za ujanja na usaliti. Aliwaambia wanaomkejeli waache kutumia mbinu za kisiasa za hadaa zinazolenga kumharibia jina na badala yake wauze ajenda zao kwa wananchi.

View Comments