In Summary

•Wawili hao walikuwa wamejihami na bastola bandia ambazo walitumia kutishia mhasiriwa ili waweze kutekeleza uhalifu huo.

•Muuza duka yule alijifanya kama kwamba ameridhishwa na simu ile na kumdanganya mshukiwa amsubiri akachukue pesa ila akaenda kufahamisha Kuria kuwa amepata mwizi wa simu yake.

Arrest

Polisi kutoka kituo cha  Murang'a wanazuilia jamaa mmoja anayedaiwa kuiba simu kisha kujaribu kuiuza tena.

Athman Karim Kori 36, alikamatwa jioni ya Jumamosi alipokuwa anajaribu kuuza simu ambayo alikuwa ameshirikiana na jamaa mwingine kuiba.

Kulingana na DCI, Athman pamoja na mwenzake walishambulia Harrison Kuria alipokuwa anaelekea nyumbani katika mtaa wa Mumbi kisha wakampora simu pamoja na shilingi 5200 alizokuwa amebeba.

Wawili hao walikuwa wamejihami na bastola bandia ambazo walitumia kutishia mhasiriwa ili waweze kutekeleza uhalifu huo.

Saa moja baadae, Athman anaripotiwa kuelekea kwa muuza duka mmoja na kumuuliza iwapo angenunua simu ile bila kufahamu alikuwa amesikia Kuria akilalamika kuwa aliibiwa simu.

Muuza duka yule alijifanya kama kwamba ameridhishwa na simu ile na kumdanganya mshukiwa amsubiri akachukue pesa ila akaenda kufahamisha Kuria kuwa amepata mwizi wa simu yake.

Kuria alifahamisha polisi ambao walifika pale dukani na kumkamata mshukiwa. Bastola bandia ambayo amekuwa akitumia kutekeleza uhalifu ilipatikana.

Mshukiwa anasubiri kufikishwa mahakamani siku ya Jumatatu huku polisi wakiendelea kusaka mwenzake aliyetoweka,

View Comments