In Summary

•Wa Iria pia aliapa hatakuwa naibu wa mgombeaji yeyote wa urais akisema anawakilisha eneo lenye kura nyingi la Mlima Kenya na wagombeaji wengine wako huru kuungana naye kuunda serikali ijayo.

•Alisema atawahamasisha wapiga kura kutoka eneo la kati kuunga mkono azma yake ya urais akizingatia kwamba kila mtu ana haki ya kidemokrasia ya kuwania kiti chochote cha kisiasa anachostahili.

Gavana Mwangi Wa Iria akihutubia waandishi wa habari
Image: BERNARD MUNYAO

Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria ameshikilia kuwa hataacha azma yake ya kuwania kiti cha juu zaidi mwaka wa 2022.

Mnamo Jumatatu, Wa Iria pia aliapa hatakuwa naibu wa mgombeaji yeyote wa urais akisema anawakilisha eneo lenye kura nyingi la Mlima Kenya na wagombeaji wengine wako huru kuungana naye kuunda serikali ijayo.

 "Siwezi kuwa naibu mtu yeyote. Kwa hakika ninatafuta uungwaji mkono kutoka kwa wagombea wengine kama Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga, kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi miongoni mwa wengine. Wacheni waniunge mkono na tuunde serikali ijayo,” alisema Wa Iria alipokutana na wakazi wengi katika uwanja wa Ihura.

Alisema atawahamasisha wapiga kura kutoka eneo la kati kuunga mkono azma yake ya urais akizingatia kwamba kila mtu ana haki ya kidemokrasia ya kuwania kiti chochote cha kisiasa anachostahili.

“Hatufai kufundishwa kuwa eneo la Mlima Kenya halifai kuwa na mgombeaji wa kiti cha urais wakati huu! Katiba iko wazi na haizuii eneo hili kutoa mgombeaji urais 2022,” alikasirisha gavana huyo.

Wa Iria ni gavana wa muhula wa pili kutoka eneo la Mlima Kenya na miongoni mwa wakuu wengine wa kisiasa wanaowania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu ujao.

"Kufikia mwaka ujao, nitakuwa nimemaliza wadhifa wangu wa sasa kama gavana wa Murang'a na kwa tajriba yangu, naweza kuliongoza taifa hili kwenye ustawi," akaongeza.

Alisema kuwa azma yake ya kuwania urais haitokani na ukabila na kudai kuwa hoja kwamba eneo la Mlima Kenya tayari limetoa marais watatu tangu uhuru haimzuilii kuwania kiti hicho.

"Haihusiani na ukabila wakati eneo la Mlima Kenya litakuwa na mgombeaji urais mwaka ujao. Mtu yeyote kutoka jumuiya yoyote ana haki ya kuwania kiti cha juu. Rais haongozi jamii bali taifa zima,” aliteta.

(Utafsiri: Samuel Maina)

View Comments