In Summary

•2NK SACCO imetupilia mbali madai kwamba ilimfuta kazi Bw Muthoni  huku ikieleza alikuwa na kesi ya kutokabidhi mwenye matatu mapato yake ya kila siku kama walivyokuwa wamekubaliana.

•Siku ya Ijumaa John Muthoni alitumia akaunti yake ya Facebook kudai alifutwa kazi punde baada ya kuripoti wanafunzi 14 ambao walikuwa wanatumia mihadarati ndani ya matatu aliyokuwa anaendesha.

Kituo cha mabasi
Image: MAKTABA

Kampuni ya usafiri ya 2NK SACCO imejitokeza kueleza kwa nini ilimimamisha kazi dereva ambaye aliripoti wanafunzi ambao walikuwa wanavuta bangi na kukata maji ndani ya matatu aliyokuwa anaendesha siku ya Ijumaa.

Kupitia taarifa ambayo ilichapishwa kwenye mtandao wa Facebook, 2NK SACCO imedai kusimamishwa kazi kwa John Muthoni hakukutokana na kitendo chake cha kuripoti wanafunzi hao wa shule ya sekondari ya Fred's Grammar ambao walikuwa wanaelekea nyumbani kwa kipindi cha likizo fupi.

2NK SACCO imetupilia mbali madai kwamba ilimfuta kazi Bw Muthoni  huku ikieleza alikuwa na kesi ya kutokabidhi mwenye matatu mapato yake ya kila siku kama walivyokuwa wamekubaliana.

"Alikuwa na kesi ya kukosa kupatia mwenye matatu mapato yake yanayotokana na nauli ya abiria. Alipoulizwa kuhusu hayo ili marekebisho yafanywe, alibishana na msimamizi wa kituo cha magari na ndio sababu akaitwa na bodi ili aeleze. Alifika mbele ya bodi na hata kukubali kuenda kuelewana na mwajiri wake kabla ya kurejea kazini" 2NK ilisema.

2NK hata hivyo imejivunia kitendo cha Muthoni cha kuripoti wanafunzi hao huku ikidai kuwa inajitolea kabisa kulinda wafanyikazi wake pamoja na waajiri.

Siku ya Ijumaa John Muthoni alitumia akaunti yake ya Facebook kudai alifutwa kazi punde baada ya kuripoti wanafunzi 14 ambao walikuwa wanatumia mihadarati ndani ya matatu aliyokuwa anaendesha.

"Mimi kama dereva wa 2NK nimepoteza kazi yangu kwa sababu ya kuripoti wanafunzi waliokuwa wanatumia bangi na pombe kwenyegari. Sasa wananinyanyasa" Muthoni aliandika.

Muthoni alikuwa anasafirisha wanafunzi 14 kutoka Karatina kuwapeleka Nairobi siku ya Ijumaa.

Walipofika eneo la Kibingoti, Muthoni alinusa harufu kali ya mihadarati aina ya bangi kutoka nyuma ya matatu yake na alipochungulia kwenye kioo cha kando akaona moshi ukitoka midomoni mwa wanafunzi ambao alikuwa amebeba huku wengine wakibugia vileo.

Alijaribu kuwasihi wakome kutumia mihadarati ndani ya gari yake ila wanafunzi wale wakaanza kumtishia na kumuagiza aachane nao na ashughulike na kuendesha gari tu.

Kutokana na ghadhabu iliyokuwa imempata Muthoni huyo aliamua kubalisha mkondo na kuelekea katika kituo cha polisi cha Sagana kupiga ripoti ila wanafunzi wale walipogundua kilichokuwa kinaendelea wakaanza kuruka mmoja mmoja kupitia kwa dirisha.

Matatu ile ilipofika katika kituo cha polisi hamkuwa na mwanafunzi yeyote ndani ila misokoto ya bangi, chupa za pombe na mizigo ambayo washukiwa walikuwa wameacha nyuma.

Kufuatia madai kwamba Muthoni alikuwa amefutwa kazi baada ya kuripoti kisa hicho, DCI Kinoti alikuwa ameomba kupatana naye .

View Comments