Afisa wa polisi aliwapiga risasi na kuwaua watu sita kabla ya kujitoa uhai katika eneo la Kabete Nairobi katika kisa cha kushangaza.
Waliofariki ni pamoja na mkewe, majirani na waendesha bodaboda ambao walikuwa wamekimbilia nyumbani kwake kuangalia kilichojiri waliposikia milio ya risasi Jumanne asubuhi.
Polisi walisema konstebo Benson Imbatu aliyekuwa akihudumu katika kituo cha polisi cha Kabete alienda nyumbani akiwa na bunduki yake aina ya AK47 na kuzua ugomvi na mkewe Carol Imbatu.
Mzozo baina yao ulibadilika kuwa mauti.
Majirani na waendesha bodaboda wanaohudumu karibu na Heights Apartment alikokuwa afisa huyo walikimbilia kwenye nyumba hiyo kuangalia kilichokuwa kikiendelea.
Hii ilikuwa baada ya wao pia kuona moto ukitoka kwenye nyumba hiyo, polisi walisema.
Na katika patashika hiyo, afisa huyo wa polisi alitoka nje akiwa na bunduki na kuanza kuwamiminia risasi watu waliokuwa nje ambapo aliua watu watano wakiwemo waendesha bodaboda wawili na majirani wake.