In Summary

• Kisa cha kwanza kilitokea katika Kituo cha Polisi cha Mtwapa ambapo afisa wa cheo cha konstebo alikamatwa baada ya kurarua Kitabu cha Matukio na kutishia kumuua OCS wa Mtwapa.

• Tukio la pili lilitokea eneo la Nkubu, Kaunti ya Meru ambapo askari polisi alikamatwa baada ya kumpiga risasi na kumjeruhi mtu mmoja kwenye kifundo cha mguu katika purukushani.

Pingu
Image: Radio Jambo

Maafisa wawili wa polisi walikamatwa katika visa viwili tofauti mijini Mombasa na Meru kwa kutekeleza uhalifu huku visa vya utovu wa maafisa wa polisi vikiongezeka. 

Kisa cha kwanza kilitokea katika Kituo cha Polisi cha Mtwapa ambapo afisa wa cheo cha konstebo alikamatwa baada ya kurarua Kitabu cha Matukio na kutishia kumuua OCS wa Mtwapa.

Polisi walisema atafikishwa mahakamani leo Jumatano na kwamba hawajui nia yake kutishia kumuua OCS.  

Tukio la pili lilitokea eneo la Nkubu, Kaunti ya Meru ambapo askari polisi alikamatwa baada ya kumpiga risasi na kumjeruhi mtu mmoja kwenye kifundo cha mguu katika purukushani. Mwathiriwa alikimbizwa hospitalini.

Wakati huo huo, Polisi wameimarisha usalama katika baadhi ya maeneo ya jiji la Nairobi kabla ya ziara iliyopangwa ya Naibu Rais William Ruto.  

Ruto anatarajiwa kuzuru maeneo ya Eastleigh, Kariobangi na Kayole ili kupata uungwaji mkono kwa chama chake cha UDA.

Polisi wameonya baadhi ya barabara huko huenda zikakumbwa na msongamano wa magari na kutaka madereva kukwepa maeneo hayo kwa muda.

View Comments