Joseph Onyango Joel Migundo mbele ya mahakama ya Milimani ambapo anashtakiwa kwa kuiba dawa kutoka KNH
Image: CAROLYNE KUBWA

Muuguzi mmoja wa hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) mwenye umri wa miaka 53 ameshtakiwa kwa kuiba dawa za thamani ya Sh81,600 kutoka hospitali hiyo.

Inasemekana kwamba Joseph Onyango Joel Migundo alipata dawa hizo kutokana na kazi yake katika hospitali hiyo. Muuguzi huyo pia anakabiliwa na shtaka mbadala la kupatikana na mali iliyoibiwa.

Inadaiwa kuwa mnamo Desemba 9, 2021, katika hospitali ya KNH, muuguzi huyo alipatikana akiwa na chupa nne za dawa hiyo inayoaminika kuwa mali ya wizi ya hospitali hiyo.

Kulingana na stakabadhi za mahakama, maafisa wa usalama wa KNH walikuwa wamepokea taarifa za kijasusi kuwa muuguzi mmoja alikuwa akiiba dawa katika kitengo cha wagonjwa mahututi hospitalini humo.

Maafisa waliokuwa katika zamu walifanya shambulizi la kuvizia kwa makusudi na ikabainika kuwa mshitakiwa alikuwa akiongeza dawa maalum katika matibabu aliyopewa mgonjwa mmoja aliyekuwa katika koma.

Inasemekana kuwa Migundo aliiba dawa hizo zilipotumwa kwenye duka la dawa kwa vile hazikuwa zimeagiziwa mgonjwa huyo kwa mujibu wa karatasi ya matibabu.

Migundo alikanusha mashtaka hayo mbele ya hakimu mkuu mwandamizi wa Nairobi Bernard Ochoi na kuachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu Sh 50,000. Kesi hiyo itatajwa Januari 27.

(Utafsiri: Samuel Maina)

View Comments