In Summary

•Wawili hao walipigwa risasi kwenye mguu kila mmoja baada ya kuiba simu ya Inspekta Elizabeth Lumumba na kukaidi amri ya kusimama.

•Wawili hao walikamatwa na waendesha bodaboda baada ya hatua chache na kupewa kichapo cha mbwa.

Bunduki
Image: Andrew Kasuku

Washukiwa wawili wa ujambazi wanaendelea kupokea matibabu maalum katika hospitali moja jijini Nairobi baada yao kujipata mashakani Ijumaa jioni walipoibia wapelelezi katika eneo la Allsopps.

Wawili hao walipigwa risasi kwenye mguu kila mmoja baada ya kuiba simu ya Inspekta Elizabeth Lumumba na kukaidi amri ya kusimama.

Kitengo cha DCI kimeripoti kwamba kwa wakati huo Inspekta Lumumba alikuwa amebebwa na koplo Hassan Mbwana kwenye gari la kibinafsi.

Baada ya kumuibia Lumumba wezi hao waliendelea kuwaibia watu wengine waliokuwa wamekwama katika msongamano wa magari kwenye barabara hiyo ya Thika Road.

Inspekta Lumumba pamoja na afisa mwingine aliyekuwa amebebwa kwenye kiti cha nyuma walishuka kutoka kwa gari lao na kuwapiga washukiwa risasi kwenye mguu walipokataa kusimama.

Licha ya kupigwa risasi washukiwa waliendelea kutoroka wakielekea Ruaraka huku waendesha bodaboda wakijiunga na maafisa hao kuwakimbiza.

Wawili hao walikamatwa na waendesha bodaboda baada ya hatua chache na kupewa kichapo cha mbwa.

Ilichukua juhudi kubwa za maafisa kutoka kituo cha Ruaraka kukomesha umati uliokuwa umejumuika kuwapiga.

Washukiwa walikimbizwa hospitalini huku wakisubiri kufikishwa mahakamani baada ya kupewa ruhuu kutoka.

View Comments